Yesu Kristo—Mwokozi wa Kipekee au Tapeli wa Kawaida? [Sehemu ya I]
Mwanafunzi mpya wa chuo kikuu aliingia kwenye darasa lake la kwanza la Dini za Kulinganisha 101. Alikuwa amekuja kwenye chuo kikuu akiwa amejiandaa—au angalau alikuwa tayari—kwa kitu chochote ambacho chuo kingemletea. Kabla ya yote, alikuwa Mkristo mwaminifu, na alilelewa na wazazi Wakristo waliojitolea, ambao wakati wa ukuaji wake, walimfundisha kuhusu Mwana wa Mungu wa kipekee, aliyetumwa kutoka mbinguni, aliyezaliwa na bikira, aliyefanya miujiza, na aliyefufuka kutoka kwa wafu, ambaye alimstahi, kumtumikia, na kumpenda. Walimu wake wa darasa la Biblia, na wahubiri ambao alikuwa akisikiliza mahubiri yao kwa miaka kumi na nane iliyopita, walimfanya pia awe na dhana kuwa hakuna mtu yeyote katika historia yote ya ulimwengu anayelingana na Yesu Kristo. Hakika, kusema kweli, mwanafunzi huyu mdogo alikua akifikiri kwamba hakuna mtu anayekaribia kufanana, au kumuiga, mwana wa seremala kutoka Nazareti.
Hata hivyo, mwanafunzi huyu alikuwa karibu kupokea mshangao wa maisha yake. Karibu siku ya kwanza ya darasa, profesa alianza kusimulia hadithi nyingi sana kuhusu “waokozi” mbalimbali wa dini nyinginezo toka zamani—inasemekana wengi wao,pia walizaliwa na mabikira, waliweza kufanya miujiza,walisulubiwa,waliokoa wanadamu, na walifufuka baada ya kifo chao. Mwanafunzi huyu wa mwaka wa kwanza hakuwa amejiandaa vizuri kumsikia profesa wake akidokeza kwamba hadithi ya Yesu Kristo kama Mwokozi wa wanadamu si ya kipekee kabisa. Kwa kweli, alishangazwa kabisa alipoona profesa akielezea ukweli kwamba hadithi za mashujaa kama hao zilikuwa zimeenea miongo kadhaa—na hata karne—kabla ya Yesu wa Nazareti kuzaliwa. Alipoona kile alichoamini kuwa ni upekee wa Bwana wake ukipotea machoni pake, kijana huyo alianza kujiuliza: Je, alifundishwa vibaya? Je, Yesu ni Mwana wa Mungu wa kipekee kweli, au alikuwa tu mmoja kati ya wahusika wengi wa zamani aliyedaiwa kuwa mwokozi binafsi wa kipekee ambaye mwishowe hakuwa hivyo? Je, hawa wengine waliodaiwa kuwa “waokozi wa kipekee” ni akina nani? Je, walikuwa wa kipekee kama walivyodai wao au wafuasi wao? Na madai haya yana athari gani kwa mafundisho ya Biblia kuhusu Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu, na imani ya mtu binafsi kwake?
Wakati wa jitihada zake za kuelewa habari mpya zilizokuwa zikitolewa kwa ustadi mkubwa (na kwa nguvu!) na profesa wake, kijana huyu alikumbana na kile kinachojulikana kama “mvutano wa utambuzi”—mkanganyiko unaotokea mtu anapokutana na habari mpya zinazokinzana na kile anachoamini kuwa ndio ukweli. Alipokuwa akijaribu kupata msimamo wa uhakika, kijana huyo alitambua kwamba alipaswa,ama kuachana na kile alichoamini kuwa ndio kweli, au kwa njia fulani kudhihirisha (na hivyo kukataa) habari mpya zinazoleta changamoto.
Kadiri alivyoendelea kuchunguza jambo hilo, ndivyo chaguo la kwanza lilivyoonekana kuwa la uwezekano mkubwa—na lisilo la kupuuzwa. Na ndivyo chaguo la pili lilivyoonekana kutowezekana. Ikiwa hali hii ingeendelea bila kukabiliwa, pingamizi lake lingefikia kiwango cha shaka kamili, na imani yake kwa upekee wa Mwokozi ambaye alimpenda na kumtii kwa muda mrefu ingefifia kabisa. Je, angeweza kusaidiwa—au isingewezekana? Je, nyenzo alizokuwa akifundishwa zilikuwa za kuaminika? Au zinaweza kupingwa—na kuweza kuiacha imani yake binafsi kwa Kristo ikiwa salama? Majibu ya maswali haya yanaunda msingi huu wa mfululizo wa makala mbili juu ya “Yesu Kristo—Mwokozi wa Kipekee au Tapeli wa Kawaida?”
NI AKINA NANI HAWA AMBAO NI “WAOKOZI WA KIPEKEE”?
Historia imejaa mifano ya wale ambao maisha yao—ni ya kweli au ni ya kufikirika—yanayoshiriki sifa Fulani, na maisha ya Yesu wa Nazareti yaliyoandikwa vizuri. Hadithi hizi mara nyingi zinajumuishwa kama sehemu ya mtaala katika kozi za kiwango cha chuo kikuu za dini za kulinganisha, na hutoa mwanzo mzuri kwa utafiti wowote kuhusu upekee wa Yesu.
Fikiria, kwa mfano, Dionysus, mungu anayejulikana sana kwa hadithi za Kigiriki. Hadithi ya kawaida ya kuzaliwa kwake inasema kuwa alikuwa mtoto wa Zeus, kiongozi wa miungu wa Kigiriki ambaye alimpa mimba mwanamke wa kibinadamu aitwaye Semele, binti wa Cadmus, Mfalme wa Thebes (ona Graves, 1960, ukurasa 56). Inasemekana Dionysus alishuka hadi kuzimu na kushinda kifo, hatimaye akamrudisha mama yake aliyekuwaamekufa kwenye nchi ya walio hai. Pia inasemekana alikufa na kufufuka tena. Wafuasi wake walimwita Lysios au Mkombozi, na juisi ya zabibu ilitumika kawaida kuashiria damu yake. Philip J. Brown alibainisha hili: “Wakristo wengi wangekuwa na hofu kufikiria kwamba kwa njia Fulani,Yesu ni sura ya Dionysus, lakini ipo mifano tata na yenye kina… Kama Yesu, Dionysus ni mungu ambaye mateso yake ya kusikitisha huadhimishwa tena kwa kula mwili wake na kunywa damu yake” (2000). Ibada ya Dionysus ilifika Roma mnamo 496 K.K., lakini ilikuwa imekwishakuwepo muda mrefu kabla ya hapo. Mfanano kati ya hadithi za Dionysus na Yesu [pamoja na ile ya Osiris, mungu wa kiume wa Misri wa uzazi na mtawala wa ulimwengu wa chini, iliyoelezewa hapa chini]—tokea kuzaliwa kwao kwa kipekee, hadi kufufuka kwao, hadi maisha yao yakikumbukwa kwa njia sawa na wafuasi wao—ni ya kushangaza kweli. Kwa kweli, katika kitabu chao cha mwaka 1999, The Jesus Mysteries, Timothy Freke na Peter Gandy walijadili kwa undani mifano kama hiyo kuunga mkono wazo kwamba Yesu wa Ukristo hakuwahi kuwepo, lakini kwa kweli alikuwa mmoja wapo tu wa wahusika wa hadithi wa zamani Waliandikwa:
Kadri tulivyoendelea kusoma matoleo mbalimbali ya hadithi ya Osiris-Dionysus, ndivyo ilivyokuwa dhahiri kwamba hadithi ya Yesu ilikuwa na sifa zote za hadithi hii ya kila mara. Tukio baada ya tukio, tuligundua kuwa tunaweza kujenga wasifu wa Yesu kutoka kwa vigezo vya hadithi vilivyowahi kuhusishwa na Osiris-Dionysus:
- Osiris-Dionysus ni Mungu aliyefanyika mwili, mwokozi na “Mwana wa Mungu.”
- Baba yake ni Mungu na mama yake ni bikira wa kibinadamu.
- Alizaliwa katika pango au zizi la ng’ombe maskini mnamo Desemba 25 mbele ya wachungaji watatu.
- Anatoa nafasi kwa wafuasi wake kuzaliwa tena kupitia ibada ya ubatizo.
- Anabadilisha maji kuwa divai katika harusi kwa njia ya miujiza.
- Anaingia mjini kwa shangwe akiwa amepanda punda huku watu wakipunga majani ya mtende kumheshimu.
- Anakufa wakati wa Pasaka kama dhabihu kwa ajili ya dhambi za ulimwengu.
- Baada ya kifo chake, anashuka kuzimu, kisha siku ya tatu anafufuka kutoka kwa wafu na kupaa mbinguni kwa utukufu.
- Wafuasi wake wanamsubiri arudi kama hakimu wakati wa Siku za Mwisho.
- Kifo chake na ufufuo wake vinasherehekewa kwa chakula cha kitamaduni cha mkate na divai, ambavyo vinaashiria mwili wake na damu yake.
Hii ni baadhi tu ya vigezo vinavyooneshwa kati ya hadithi za Osiris-Dionysus na wasifu wa Yesu. Kwa nini mifano hii ya kushangaza haijulikani kwa kawaida? (ukurasa 5).
Hata hivyo, Dionysus si pekee mwenye hadithi kutoka zamani zinazofanana na ya Yesu. Prometheus ni mungu mwingine wa hadithi ambaye alipitia kifo kinachofanana na cha Kristo. Hadithi yake ilianza kuzunguka mnamo 547 K.K.
Au, fikiria Krishna, mungu wa kale wa Kihindu ambaye anasemekana kuwa na hatima inayofanana na ile ya Kristo. Ameoneshwa akiwa amesulubiwa, na matundu mikononi na miguuni mwake. Hadhi yake? ……”Bwana Wetu na Mwokozi.” inasemekana Krishna “alifufuka kutoka kwa wafu” na kisha “kupaa kimwili mbinguni” (Doane, 1882, ukurasa 215).Hata inasadikika akisema: “Fanya mema kwa ajili yake mwenyewe, na usitarajie malipo yake duniani” (Graves, 1875, ukurasa. 112). Kristo alitumia wazo lile lile katika Mathayo 6. Lakini hadithi ya Krishna ilianzia mwaka 1200 K.K.
Mifano inaendelea. Katika Papyrus ya Ani ya Wamisri (inayojulikana pia kama Kitabu cha Wafu cha Wamisri), ambayo ina nyakati kati ya 1450 na 1400 K.K. (tazama Budge, 1960, ukurasa 220), mungu Osiris anaitwa Majina ya Wafalme, Bwana wa Mabwana, na Mkuu wa Wakuu (Budge, uk. 352). Katika kitabu chake cha kuvutia, Bible Myths and Their Parallels in Other Religions, T.W. Doane alibainisha: “Osiris, Mwokozi wa Misri, baada ya kuuawa, alifufuka kutoka kwa wafu, na alipewa jina la ‘Aliyefufuka‘” (ukurasa 221, msisitizo kwenye asili). Karani wa Osiris, Ani, anafafanuliwa kama mmojawao “ambaye neno lake ni kweli” (Budge, ukurasa 384). Katika sehemu ya mwisho ya papyrus, kuna kanuni maalum iliyotolewa, ambayo inasemekana kuwa na uwezo wa kutoa haki kwa mtu anayeisoma wakati wa kuingia kwake kwenye umilele. Kanuni hiyo inasomeka kama ifuatavyo: “Nimewapa mkate wenye njaa, na maji kwa yule aliyekuwa na kiu, na nguo kwa mtu aliyekuwa uchi, na mashua kwa yule ambaye hakuwa na mashua” (Budge, ukurasa 587). Mwandishi wa papyrus hii ni kama alinakili maneno ya Yesu kama yalivyo katika Mathayo 25:31-46—isipokuwa kwa ukweli mmoja mdogo: Papyrus ya Ani ina tarehe ya 1400 K.K.—zaidi ya miaka elfu moja kabla ya Kristo kufanya maonesho yake duniani.
Aidha, mnamo mwaka 550 K.K., Confucius alisema: “Usifanye kwa mwingine usichotaka kufanyiwa wewe mwenyewe.” Kristo alitoa tamko karibu sawa takriban miaka 600 baada ya Confucius kunena hivyo: “Na kama mnavyotaka watu wawatendee, watendeeni vivyo hivyo” (Luka 6:31).
Mifano pia ipo kati ya hadithi za Buddha na Yesu. Katika makala ya jalada aliloandika katika toleo la Machi 27, 2000 la Newsweek kuhusu “Yesu Mwingine,” Kenneth L. Woodward alibaini kwamba “hadithi za maisha ya Yesu na Buddha zinafanana sana,” na kisha akaendelea kubainisha kwamba viongozi hawa wa dini walipinga mafundisho ya kidini ya wakati wao, inadaiwa walizaliwa na mabikira, na walipaswa kufanya miujiza (135[13]:58-59).
Baadhi ya wakosoaji wa Biblia wanapendekeza kuwa ni jambo rahisi tu kutoa hadithi zenye kufanana kama hizi kwa wingi. Kwa kweli, katika mjadala wa hadhara na mwanatheolojia Norman Geisler (uliofanyika katika Chuo cha Columbus huko Columbus, Georgia mnamo Machi 29, 1994), Farrell Till, ambaye alikuwa Mkristo aliyegeuka kuwa msomi mkosoaji, alisema hivyo hasa alipowaambia wasikilizaji:
Watu, ninataka muache na kufikiria kwa uzito kwa muda mfupi. Najua ni kiasi gani cha hisia kinahusishwa na hili, lakini tafadhali eleweni hili. Miungu waliofufuka na kuokolewa, ambao walizaliwa na mabikira, walikuwa wa kawaida sana wakati huo (1994).
Stephen Franklin—ingawa ni mtetezi mwenye bidii, wa upekee wa Kristo—alithibitisha kauli ya Till katika makala, katika Evangelical Review of Theology aliposema: “Kupatikana kwa mwili, mbali na kuwa pekee kwa Ukristo, inaonekana kuwa urithi wa kidini wa binadamu” (1993, ukurasa 32).
Wakosoaji wa Kristo wamekuwa wakitumia mifano kama hiyo mara kwa mara katika jaribio la kudhihirisha dai lao kuwa Yesu wa Nazareti si mhusika wa kipekee wala mwokozi binafsi anayestahili. Kwa mfano, majuma matatu baada ya makala ya Kenneth Woodward kuhusu Yesu,kuchapishwa katika Newsweek, barua kwa mhariri kutoka kwa Don Zomberg wa Wyoming, Michigan ilionekana katika toleo la Aprili 20 la jarida hilo. Katika kujibu nukuu kutoka makala ya Woodward ambayo ilipendekeza kwamba “Kristo ni wa kipekee kabisa,” Bw. Zomberg aliandika kupinga aliposema: “Hakuna kitu kinachoweza kuwa mbali zaidi na ukweli. Hadithi ya Yesu ni tofauti kidogo na ya dini za zamani za Mashariki ya Kati zilizokuwepo miaka elfu kadhaa iliyopita” (2000, 135[16]:17). Mtazamo kama huo unatokana na ukweli kwamba mifano ya kihistoria na ya hadithi kati ya Yesu na watu wengine wa kidini ipo, na inawezekana ni maarufu zaidi kuliko vile watu wengi wanavyofikiria. Na ingawa ni ukweli kwamba hakuna hata moja ya mifano hii ya kihistoria/ya hadithi inayofanana kabisa, ni ukweli kwamba zinakaribia kukamilika kwa kuleta uchunguzi makini kwa wale wanaoamini kuwa, Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu wa kipekee.
Kwa kweli, wakosoaji wa kisasa ambao hutumia hoja kama hiyo katika majaribio ya kupinga upekee na uungu wa Kristo hawawezi kuchukua sifa kama waanzilishi wake. Historia inaonesha kuwa karibu miaka elfu mbili iliyopita, watetezi wa kristo wa mapema walikuwa wakijihusisha kwa bidii na kujibu hoja hiyo hiyo. Kwa mfano, Augustine wa Hippo (A.D. 354-426) alisema katika kitabu chake cha Christian Doctrine:
Wale wasomaji na wapendwa wa Plato walithubutu kudai kwa uwongo kwamba, Bwana wetu Yesu Kristo alijifunza maneno yake yote, ambayo wanalazimika kuyakubali na kuyasifu, kutoka kwenye vitabu vya Plato kwa sababu (walidai) haiwezi kukataliwa kwamba Plato aliishi muda mrefu kabla ya kuja kwa Bwana wetu (2:28, kipengele cha mabano kwenye asili.).
Augustine alikanusha hoja hiyo kwa kubainisha kwamba, Plato alisoma toka kwa nabii Yeremia kisha kwa urahisi akaingiza mafundisho ya Yeremia katika mafundisho yake mwenyewe. Hata hivyo Hoja hiyo,ni wazi: mapema kama A.D. 400, wakosoaji na maadui wa Msalaba walikuwa wakipambana vikali kwa mishale mikali ya madai ya wizi wa maandishi kwa Kristo na wafuasi wake.
Uchunguzi zaidi katika historia ya utetezi wa Kikristo unaonesha jambo la kushangaza zaidi. Watetezi wa awali sio tu kwamba walitambua kuwa hadithi na mafundisho ya Yesu kuwa yanafanana sana na hadithi za zamani za kihistoria, bali hata walisisitiza kufanana huku kwa jaribio la kuwafanya wapagani kuelewa zaidi kuhusu Yesu na ujumbe wake. Justin Martyr (A.D. 100-165) alitoa hoja katika First Apology yake ambayo ilikusudiwa kumuweka Kristo angalau kwenye uwanja sawa na miungu ya zamani ya hadithi za kale.
Na ikiwa tunadai kwamba Neno la Mungu alizaliwa na Mungu kwa njia ya kipekee, tofauti na uzazi wa kawaida, acha hii, kama ilivyoelezwa hapo juu, isiwe jambo la ajabu kwenu, mnaosema kwamba Zebaki ni neno la malaika wa Mungu. Lakini ikiwa mtu yeyote anapinga kwamba Alisulubiwa, katika hili pia Yeye ni sawa na wale wanaodhaniwa kuwa wana wa Mshtarii (Jupiter) wa kwenu…. Na ikiwa tunasema kwamba Alizaliwa na bikira, pokeeni hii kama vile mnavyokubali kuhusu Ferseus. Na katika kusema kwamba Aliwaponya vilema, waliopooza, na wale waliozaliwa vipofu, tunaonekana kusema kile kinachofanana sana na matendo yanayosemekana kufanywa na Æsculapius (Sura ya 22).
Tertullian (takriban A.D. 160-220) aliona kwamba hadithi ya Romulus, muhusika mwingine kutoka katika hadithi za kale za Kigiriki ambaye alijulikana baada ya kifo chake, ilikuwa sawa kabisa na hadithi ya Kristo kufahamika zaidi baada ya kifo chake. Hata hivyo, Tertullian aliendelea kubainisha kwamba hadithi za Kristo zilikuwa na uhakika zaidi kwa sababu zilikuwa zimeandikwa na ushahidi wa kihistoria (Apology, 21).
Wakati wapagani wa zamani walipoona,na wakosoaji wa kisasa bado wanaona, mifano kama hiyo kama inavyopingana na upekee wa Kristo, maandiko ya watu kama Augustine, Justin Martyr, Tertullian, na wengine yanaonesha ukweli kwamba Wakristo wa kale waliona ndio wazi,kukaribisha hata mifano kati ya hadithi ya Yesu na hadithi za miungu wa wapagani. Aidha, baadhi ya Wakristo hao wa kale walikumbatia mifano hiyo hiyo kutetea nafasi ya Yesu kama Mwana wa Mungu wa kipekee. Hoja ya watetezi hao, bila shaka, ilikuwa ya pande mbili: (1) watu wa zamani waliokuwa wamemtafuta mungu mwokozi wa kipekee na, kwa kutomkuta, walifikia hatua ya kumuumba na kumpa sifa maalum; na (2) kwamba Mwokozi ambaye, ingawa zamani alikuwa amepewa sifa za kipekee kutokana na ubunifu wao dhaifu kwa kweli alikuwepo!
Wakristo wanapaswa kuutambua kama ukweli usiopingika,ukweli uliothibitishwa na hadithi za kale, historia, na hata watetezi wa Kikristo waliotangulia.Kwamba hati za kale zinaonesha kuwa hadithi ya Kristo si hadithi ya kwanza kabisa kuhadithiwa dhidi ya mungu mwokozi aliyezaliwa na bikira, aliyesulubiwa, kufufuliwa, mwenye kufanya miujiza ambaye alidaiwa kufa kwa ajili ya dhambi za wanadamu. Hati hizi pia zinaonesha kuwa mafundisho mengi ya Kristo wakati mwingine yanaweza kuondolewa karibu kama ilivyotoka kwenye vyanzo ambavyo vilikuwa vikizunguka mamia au maelfu ya miaka kabla ya Yesu kuzaliwa. Watetezi wa hapo awali walikubali ukweli huu kwa sababu walikuwa na nia ya dhati kabisa.
Na hiyo inaturudisha kwenye suala lililokuwa likimsumbua mwanafunzi wa chuo aliyetajwa mapema. Je, tunawezaje kuthibitisha kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu wa kipekee, wa kweli—wakati hadithi zinazofanana na Yake zilisambazwa miongo kadhaa au milenia kabla Yeye hajawahi kuja Duniani? Tunaweza kutoa jibu gani kwa madai ya wakosoaji wa Biblia? Na tunaweza kutoa uhakikisho gani kwa mwanafunzi huyo mchanga kuhusu ukweli wa imani yake?
KWANINI YESU ASIWE WA KIPEKEE?
Kabla hatujashughulikia swali kuu la mfululizo huu wa makala mbili, swali la wazi lazima liulizwe: Kwanini mtu yeyote atake kudai kwamba hadithi ya Yesu si ya kipekee au ni wizi wa maandishi? Kuna majibu kadhaa ambayo yanaweza kutolewa kutokana na swali kama hilo. Kwa sababu ya kizuizi cha nafasi, hata hivyo, tungependa kuzingatia majibu mawili tu. Kwanza, ni ukweli rahisi kwamba wale ambao hawamuamini Mungu,wanakubali mtazamo wa kiasili kabisa wa asili ya Ulimwengu na wakazi wake, lazima wapate njia ya kuelezea upekee wa Kristo na upekee wa mfumo wa dini aliyoianzisha. Katika kushughulikia suala hili, marehemu James Bales aliandika:
Ikiwa mtu anakubali maelezo ya kiasili na ya mageuzi ya asili ya dini, ataamini kwamba Ukristo unaweza kuelezeka kiasili. Mbinu yake yenyewe imeondoa uwezekano wa ufunuo wa kimuujiza wa Mungu katika Yesu Kristo (ukurasa 7).
Mwana uyakinifu maarufu wa Uingereza Sir Julian Huxley aliweka bayana:
Katika mtazamo wa mageuzi ya fikra hudai kwamba, hakuna tena haja au nafasi ya miujiza.Pia Dunia haikuumbwa;bali ilibadilika. Vivyo hivyo wanyama na mimea yote inayokaa ndani yake, pamoja na nafsi zetu za kibinadamu, akili, na roho vile vile ubongo na mwili. Vivyo hivyo na dini (1960,ukurasa 252-253, msisitizo umeongezwa).
Wale wanaoamini kwamba Ulimwengu na maisha kwa ujumla ndani yake yalibadilika kwa njia ya asili kabisa. pia lazima wapate sababu ya ya msingi kabisa kwa kila kipengele cha maisha.Hata dini ni mojawapo ya vipengele hivyo, na kwa hiyo, kulingana na mwelekeo wa asili,pia lazima iwe imebadilika hasa kama Huxley alivyopendekeza ilivyokuwa hapo awali. Sio ngumu kuona ni kwa nini mwanauyakinifu alivyoamini kuwa ni lazima hadithi ya Yesu itokane na hadithi za zamani, za awali. Kwa kweli, kusema kwamba hadithi ya Yesu “ilibadilika” kutoka kwenye hadithi za zamani yaani za awali,hii ni kusema kwamba, kitu kisichozidi ile nadharia ya mageuzi tayari kinafundisha katika kila eneo alipo binadamu. Mwanafalsafa Joseph McCabe alieleza: “Kile tunachokiona, kwa kweli, ni mageuzi katika dini. Mawazo hupitishwa kutoka kizazi hadi kizazi, akili hapa na akili pale huongeza au kuboresha kidogo. Mto wa polepole wa mageuzi ya binadamu umeingia kwenye mawimbi yake” (1993, ukurasa 72, msisitizo umeongezwa).
Pili, wakati mwingine baadhi wanaweza kupotoshwa na utafutaji wa asili ya dini, wengine wanafundisha kwamba hadithi ya Yesu ilitokana na hadithi za zamani za Kiyahudi na/au za kipagani. Kama vile Bales alivyobainisha.Na baadhi wamependekeza kwamba, “Kristo na Ukristo vinatazamwa kama maendeleo ya kawaida tokea kwenye Uyahudi na upagani” (ukurasa 7). Nia hiyo hiyo imetetewa na wale waliokuwa waumini na baadaye kuasi, Timothy Freke na Peter Gandy, katika The Jesus Mysteries (ambalo ni shambulio wazi kabisa, mbele ya uungu wa Kristo).
Sote wawili tulilelewa kama Wakristo na tulishangazwa na kugundua kwamba, licha ya miaka ya uchunguzi wa kiroho ulio wazi, bado kwa namna fulani ilihisi kuwa hatari hata kuthubutu kufikiria mawazo kama hayo. Mafundisho ya awali hufika kwa kina. Kwa kweli tulikuwa tukisema kwamba Yesu alikuwa mungu wa Kipagani, na kwamba Ukristo ulikuwa matokeo ya uasi wa Upagani! hili lilionekana kuwa la kushangaza. Hata hivyo nadharia hii ilielezea kwa urahisi na kwa uzuri, mifano kati ya hadithi za Osiris-Dionysus na Yesu Kristo ni sehemu ya hadithi mojawapo inayokua….
Hadithi ya Yesu ina sifa zote za hadithi, kwa hiyo inawezekana kwamba hiyo ndiyo sahihi… Kwa nini tuchukue hadithi za Osiris, Dionysus, Adonis, Attis, Mithras, na waokozi wengine wa Kipagani kama hadithi, lakini pia tukutane na hadithi hiyo hiyo katika muktadha wa Kiyahudi na kuamini kuwa ni wasifu wa seremala kutoka Bethlehemu?…
Tumeamini kwamba hadithi ya Yesu si wasifu wa Masihi wa kihistoria, bali ni hadithi inayotokana na hadithi za kale za Kipagani. Ukristo haukuwa ufunuo mpya na wa kipekee bali ilikuwa mabadiliko ya dini ya kale ya Kiyahudi, ya Kipagani,na ya Siri. Hii ndiyo tunayoita Tasnifu ya Siri za Yesu….
Maelezo dhahiri ni kwamba kadri Ukristo wa kale ulivyokuwa na nguvu kubwa katika ulimwengu uliokuwa wa Kipagani hapo awali, mitindo maarufu kutoka kwenye hadithi za Kipagani ziliongezwa kwenye wasifu wa Yesu…. Mitindo kama hiyo ilikopwa kutoka katika Upagani kwa njia ile ile ambayo sherehe za Kipagani zilichukuliwa kama siku za watakatifu wa Kikristo…. Hadithi ya Yesu ni hadithi ya milele…si hadithi tu ya matukio yaliyotokea kwa mtu fulani miaka 2,000 iliyopita (1999, uk. 9-10,2,6,13, msisitizo kwenye asili.).
Na kwa hivyo, ingawa inaweza kuwa kulikuwa na mtu halisi anayejulikana kama “Yesu Kristo,” huyo hakuwa zaidi ya kristo—tena mtu. Sifa alizodaiwa kuwa nazo na wafuasi wake (mfano, upekee wa kuingia kwake duniani, upekee wa shughuli za safari zake hapa duniani,upekee wa kuondoka kwake hapa duniani, n.k.) hizo zote zilitoka “baada ya tukio” kutokana na kukopwa kutoka katika vyanzo vya kale vya kipagani na/au Kiyahudi.
Sio ukweli wa kihistoria wa Kristo unaokuwa kwenye mizani hapa (angalia, kwa mfano, mwandishi Butt, 2000); wasioamini na makafiri wa kila aina wamekiri kuwepo Kwake kwa muda mrefu. Badala yake, suala linahusiana na kama Yesu wa Nazareti alikuwa ni yule aliyedai kuwa—Mwana wa pekee wa Mungu aliyefanyika mwili.
IDARA YA KIDINI YA MWANADAMU NA “UFANANISHO WA MWOKOZI”
Ukweli wa mambo ni kwamba,hadithi nyingi katika historia zinafanana na ile ya Yesu wa Nazareti kwa namna moja au nyingine. Na kwa nini hili litushangaze? Baada ya Adamu na Hawa kula tunda kutoka kwenye mti wa ujuzi wa mema na mabaya, mwanadamu alitambua kwa kina uwepo wa dhambi na matokeo yake. Tangu wakati wa Kaini na Abeli, Mungu aliweka dhabihu na kuamuru sheria maalum kuhusu dhabihu hizo. Tangu wakati huo, wanadamu wote wamekuwa na angalau ufahamu Fulani hata kama ni mdogo au uliopotoka.kwamba wanahitaji “kufanya kitu” ili kusimama wakiwa wameheshimika mbele ya Muumba wao. Njia moja ya kufanya hivyo ilikuwa ni kubuni “mwakilishi” mwenye kuweza kuchukua nafasi yao kama mfano wa ukamilifu usio na dhambi ili kuomba kwa niaba yao mbele ya Hakimu Mwenye Haki wa Dunia yote (Mwanzo 18:25).
Zaidi ya hayo, hata hivyo, inaweza kusemwa kwamba ufanano tulioutaja (na, kwa hakika, mwingine mwingi kama huo) ni ufanano tu, si sawa kabisa. Pia Inaweza kusemwa kwamba hadithi ya Yesu, ingawa inaonekana kufanana na baadhi ya hadithi nyingine, si sawa kabisa na, kwa kweli, inatofautiana sana katika maelezo madogo. Kwa mfano, Krishna anadaiwa alisulubiwa kwa njia ya mshale kupitia mikononi mwake, wakati, Yesu aligongelewa misumari kwenye msalaba. Confucius yeye alitoa umbo hasi ya kile kinachoitwa “kanuni ya dhahabu” (“Usiwatendee wengine”), wakati Yesu alisema chanya (“Watendee wengine”). Mama yake Dionysus, Persophone, inasemekana alifanya ngono na Zeus, wakati Maria alikuwa bikira. Mstari huu wa hoja una uzito fulani, kwa sababu hakika ni kweli kwamba hakuna hadithi yoyote ya zamani inayosikika kabisa kama ile ya Kristo.
Mwenendo wa hivi karibuni wa hadithi ya Osiris wa Misri unatoa mfano mzuri wa tofauti nyingi muhimu kati ya simulizi ya Yesu na hadithi nyinginezo. Hadithi inasema kwamba Osiris aliuawa na kaka yake mwovu Seth, ambaye alirarua mwili wa Osiris vipande kumi na nne na kuvitawanya kote Misri. Isis, mungu-mke-mwenza wa Osiris, alikusanya vipande hivyo na kuvipeleka, na hivyo kumpa uhai Osiris katika ulimwengu wa chini. Baadaye, alitumia ujuzi wa kichawi kumfufua Osiris na kumzaa mtoto (Horus) naye. Baada ya kumzaa Horus, Osiris alibaki katika ulimwengu wa chini, hakurudi tena kwa wafu (Encyclopaedia Britannica, 1997, 8:1026-1027). Hadithi hii, ikichukuliwa kwa ujumla, haitoi ufananisho halisi wa hadithi ya Yesu. Aidha, hadithi zote kuhusu wahusika ambao inasemekana walikuwa sawa na Kristo zinapozungumziwa kwa ukamilifu wake, ni wazi kwamba kila moja ina sifa chache tu zinazokaribia kufanana na zile zilizomo katika hadithi ya maisha ya Yesu. Aidha, baadhi ya mfanano unaodaiwa unategemea nyaraka dhaifu na huenda hata ukawa umebuniwa.
Hata hivyo, kuna kauli fulani za kawaida zinazotumika katika hadithi mbalimbali:Kimsingi shujaa wa ajabu hufanya mambo ya miujiza, huuawa ili kuokoa binadamu (wakati mwingine hata kwa kusulubiwa), na hufufuliwa kwa namna moja au nyingine, hivyo kushinda kifo. Ingawa maelezo madogo ni tofauti kabisa, ufanano wa jumla ni wa karibu vya kutosha kudai uchunguzi—na maelezo. Kwa mfano, hebu fikiria mtu fulani akichukua makala yetu iliyohifadhiwa kisheria,akatumia kamusi kubadilisha mamia ya maneno yake, na kisha kuweka jina lake bila ya sisi kujua au kutoa idhini. Tutamuona mtu huyo kama mwizi wa wazi. Ingawa makala mpya inaweza kuwa “ya kipekee” katika madogo yake, kwa ujumla bado itakuwa nakala. Kwa njia sawa, haitoshi Wakristo kudai kwamba hadithi ya Yesu haikutokana na moja (au zaidi) ya hadithi za kale kwa kusema tu kwamba maelezo madogo ya maisha Yake ni tofauti na mengine. Lazima tutoe hoja bora, ya kina zaidi, na ya kusadikisha zaidi kuliko hii ikiwa hadithi ya Yesu Kristo itatetea kuwa ya kipekee.
Asili Huru inayohusu za Mfanano wa Hadithi
Katika sehemu ya mwanzo mwa karne ya ishirini, Joseph McCabe, mmoja wa waasi waziwazi wa siku zake, alichapisha kazi kadhaa, zikiwemo The Myth of the Resurrection (1925), Did Jesus Ever Live? (1926), na How Christianity “Triumphed” (1926). Mnamo mwaka wa 1993, Kampuni ya Uchapisaji ya Prometheus (zingatia kwamba jina la shirika hili la uchapaji la kidunia ni jina la mmoja wa miungu wa Kigiriki anayesemekana kuwa na sifa zinazofanana na za Yesu) ilichapisha upya kazi hizi katika kitabu kilichoitwa The Myth of the Resurrection and Other Essays. McCabe aliandika kwa uangalifu ulinganifu kati ya hadithi za Yesu na hadithi za kipagani kama vile za Osiris, Adonis, Tammuz, na Attis, lakini alionesha maalum: “Ni kipengele muhimu sana cha hadithi yetu kwamba hadithi hii ya mungu aliyeuawa na kufufuka ilijitokeza katika sehemu tofauti kabisa za ulimwengu wa zamani wenye tamaduni za kistaarabu.” Tammuz, Attis, na Osiris ni viumbe watatu tofauti na huru wa mawazo ya hadithi” (1993 ukurasa 45, imesistizwa). McCabe alikubali kwamba hadithi hizi za kipagani zenye mada zinazofanana hazikukopi nyingine au hadithi moja ya mapema, bali zilijitokeza kwa kujitegemea—na hata kwa uhuru—kutoka kwa kila mmoja wao. McCabe alikiri: “Kwa sababu fulani… akili ya mwanadamu ilifika katika sehemu nyingi za dunia kufikiria hadithi ya kifo na ufufuo…. Kwa kweli, katika namna moja au nyingine kulikuwa na imani karibia ulimwengu mzima kwamba Mungu, au mwakilishi [mfalme, mfungwa, sura, nk.] wa Mungu, alikufa, au alilazimika kufa kila mwaka” (ukurasa 52,53, imesistizwa; vitu vilivyowekwa ndani ya mabano vilikuwepo kwenye asili). Katika hitimisho lake, McCabe aliandika: “Kwa muhtasari, ningesema kwamba imani ya ulimwengu mzima katika mungu aliyeuawa na kufufuka inatoa mwanga kwa imani ya Kikristo kwa kuonyesha hali ya kiakili ya ulimwengu ambayo kwa urahisi, katika sehemu nyingi, ilifanya hadithi ya ufufuo” (ukurasa 63, emph. iliyoongezwa). McCabe—hata kama yeye ni mkatili—aliridhia kwamba hadithi nyingi (lakini tofauti) za ufufuo zilijitokeza kutoka maeneo mbalimbali duniani, kila moja ikiwa na ukweli wa kufanana lakini asili yake ikawa tofauti. Hadithi hizi zinaonekana kujitokeza kwa sababu ya kile alichokiita “hali ya kiakili ya ulimwengu.” Na hata hivyo licha ya ushahidi kama huo, katika ukurasa wa 69 wa kitabu chake, McCabe alihitimisha: “Mwanadamu hana hamu ya kidini.”
Silika ya Kidini ya Binadamu
Kwa sababu ya “mfumo wa akili wa ulimwengu”,duniani kote kwa uhuru Watu walibuni hadithi zinazohusiana na mungu anayekufa kisha kufufuka. Hadithi hizi zinavuka vizuizi vya wakati na mipaka ya kijiografia; ni kwa maana halisi sana ulimwenguni kote.Lakini tunaombwa kuamini kwamba watu kutoka nchi na tamaduni mbalimbali waliobuni hadithi hizi walikuwa na mtazamo wa kwamba “hakuna silika ya kidini”? hivi ndivyo McCabe alivyoweza kufanya makubaliano aliyoyafanya, lakini akafikia hitimisho kama hilo,kwamba ni vigumu kueleweka kwa njia ya busara.
Kiuhalisia, mwanadamu ana silika moja ya kidini ambayo ni kali zaidi kuliko hata ya wanateolojia wengiambao wangependa kukubali. Akizungumza juu ya Mungu, mwandishi wa Muhubiri alisema: “Amefanya kila kitu kuwa kizuri kwa wakati wake: ameweka umilele mioyoni mwao” (3:11). Paulo alisema kwamba wanadamu daima wameweza kuelewa “uwezo wa milele na uungu” wa Mungu (Warumi 1:20). Mungu hakumweka mwanadamu duniani ili kumuacha. Badala yake:
Alifanya kwa ajili ya kila taifa la wanadamu kukaa juu ya uso wa dunia yote, akiwa ameamua nyakati zao na mipaka ya makao yao; ili wamtafute Mungu, kama ikiwezekana wamshike na kumwona ijapokuwa hayuko mbali na kila mmoja wetu; kwa maana ndani yake tunaishi, na tunatembea na kuwa na maisha yetu; kama baadhi ya washairi wenu walivyosema, kwa maana sisi ni uzao wake” (Matendo 17:26-28,msisitizo umeongezwa).
Mungu kwa hakika ameweka umilele mioyoni mwa watu na kuwapa silika ya ulimwengu ambayo imelenga kuwafanya wamtafute Yeye.
Katika kitabu chake, Why We Believe the Bible, marehemu George DeHoff alitoa maoni: “Hakuna taifa au kabila lililopo ambalo halikuamini katika Kiumbe Mkuu wa aina fulani na kufanya dini kwa namna fulani” (1944, ukurasa 42).Yuko sahihi kabisa. Lakini siyo wanaoamini tu ambao wamewasilisha na kutoa ushahidi wa aina hii.Bali hata wale wasioamini wamelazimika kufikia hitimisho hilo kutokana na ushahidi wa kihistoria na kisayansi.
Zaidi ya miaka sabini iliyopita, Clarence Darrow na Wallace Rice waliungana kuhariri kitabu kilichoitwa Infidels and Heretics: An Agnostic’s Anthology. Kwenye kurasa za ndani, maelezo ya kitabu yaliyomo yalieleza kuwa kulikuwa na “mavuno bora zaidi kutoka kwenye kazi muhimu zaidi za wasomi wakubwa, wenye mashaka, wasioamini na wazushi wa dunia.” Katika ukurasa wa 146, wahariri walimnukuu mpingaji maarufu, John Tyndall:
Dini haiishi kwa nguvu na msaada wa kanuni, bali kwa sababu imejiegemeza katika asili ya mwanadamu. Ili kufafanua kwa kutumia mfano wa usanifu, miundo imeharibiwa na kujengwa tena mara kwa mara, lakini madini yaliyojaa moto yanaendelea kuwepo katika kikombe cha ubinadamu. Mshikamano wa kina na wa kudumu hauwezi kupotea hivi karibuni… (1929).
Takribani miaka hamsini baadaye, Edward O. Wilson wa Chuo Kikuu cha Harvard (ambaye anajulikana kama “baba” wa taaluma ya Kijamii) aliandika kitabu kiitwacho On Human Nature. Ndani mwa Jalada la mbele kilieleza kuwa lengo la Wilson lilikuwa “sio tu kukamilisha mapinduzi ya Darwin kwa kuleta mawazo ya kibaiolojia katikati ya sayansi ya jamii na ubinadamu.” Wilson aliandika: “Mwelekeo wa kuamini katika dini ni ngumu na wenye mkanganyo katika akili ya mwanadamu, na kwa uwezekano wote sehemu isiyoweza kuondolewa ya asili ya binadamu” (1978, ukurasa 167). Aliendelea kusema kwamba “wasiomwamini Mungu wanaendeleza imani kwamba sayansi na maarifa yatafukuza dini, ambayo wanaichukulia kuwa sio zaidi ya utando wa udanganyifu,” lakini wazo kwamba kuongezeka kwa maarifa na teknolojia kutaondoa asili ya kidini ya mwanadamu “haijawahi kuonekana kuwa ya kijinga zaidi kama ilivyo leo” (ukurasa 170).
DHABIHU KAMILI
Je, basi, ni vipi hisia ya kumwabudu Mungu ilivyopelekea kuibuka kwa hadithi nyingi kuhusu mungu-mwokozi aliyezaliwa na bikira ambaye hufa kama dhabihu kwa ajili ya dhambi za wanadamu? Kwanza, ilianza na wazo la dhabihu. Tangu wakati Adamu na Hawa walipofukuzwa kutoka Bustani ya Edeni, mwanadamu alikuwa na ufahamu mkali kwamba yeye ni kiumbe mwenye dhambi anayehitaji ukombozi. Wanadamu pia walielewa kwamba aina fulani ya dhabihu ya upatanisho ilikuwa inahitajika ili kuwaondolea dhambi. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania aliona kwamba “kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini” (11:4). Cha ajabu, wakosoaji wanaonekana kuelewa jambo hili vizuri sana. Mwishoni mwa karne ya kumi na tisa, T.W. Doane aliushambulia kwa kejeli mafundisho ya Kristo na Biblia. Kazi yake, Bible Myths and Their Parallels in Other Religions (1882), iliuvunja kila msingi wa mafundisho ya Kikristo. Hata hivyo, hata yeye alielewa kwamba wanadamu siku zote wamekuwa wakitambua dhambi zao wenyewe na hitaji lao la dhabihu ya upatanisho. Aliandika: “Mafundisho ya upatanisho wa dhambi yalikuwa yamehubiriwa muda mrefu kabla ya mafundisho hayo kufafanuliwa kutoka kwenye Maandiko ya Kikristo, muda mrefu kabla ya Maandiko haya kudaiwa kuandikwa” (ukurasa 181). Msomi wa Biblia R.C. Trench alitoa maoni:
Mataifa ambayo hayawezi kujifunza kutoka kwa mwingine, mataifa yaliyo tofauti zaidi katika tamaduni, yaliyo juu zaidi katika kiwango na karibu chini zaidi, yanatofautiana katika kila kitu isipokuwa jambo hili moja, yaani, katika kutoa vitu vilivyo na uhai kwa Mungu,—au, ambapo wazo la Mungu mmoja limepotea,—kwa ‘miungu mingi’ ya wapagani—kipengele muhimu cha sadaka hiyo katika kila hali ni kwamba uhai wa mnyama ulipeanwa” (ukurasa 177).
Wale ambao wangependa kupinga tathmini ya Trench wanaweza kuchunguza kitabu chochote cha historia ya dunia au dini za ulimwengu na kuona kwamba yuko sahihi. Abeli alitoa kwanza wa kundi lake, na tangu siku hiyo kuendelea, wanadamu walianza kutoa dhabihu za uhai kwa mungu kwa matumaini ya kuzuia hasira na kusamehewa dhambi. Kwa kweli, wanadamu wametoa dhabihu za viumbe hai kwa mungu tangu mwanzo wa wakati. Lakini ni dhabihu zipi hasa ambazo wanadamu walifikiri zilikuwa na nguvu ya kusamehe dhambi? Kanuni ya jumla kwa thamani ya upatanisho wa dhabihu ilikuwa: dhabihu inayogharimu zaidi na kamili, ndivyo dhambi zaidi itakavyoondolewa.
Mungu alipoweka ibada ya dhabihu za wanyama kwa ajili ya sherehe za kidini za watu wake wateule, aliweka sheria kali. Katika Mambo ya Walawi 22:19-20, Mungu aliwaambia Wayahudi: “Mtatoa kwa hiari yenu mnyama mume asiye na dosari kutoka kwa ng’ombe, kutoka kwa kondoo, au kutoka kwa mbuzi.Lakini chochote kilicho na dosari, hamtakitoa, kwa maana hakitakubalika kwa niaba yenu” (NKJV). Bwana daima amedai kwamba damu imwagike kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Waebrania 9:22 inasisitiza hoja hiyo: “Na kwa mujibu wa sheria…vitu vyote vinatakaswa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.” Hili halipaswi kushangaza kabisa, kwani “uzima wa mwili uko katika damu, nami nimewapa hiyo juu ya madhabahu ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu: kwa maana ni damu inayofanya upatanisho kwa sababu ya uzima” (Mambo ya Walawi 17:11).
Wanaume na wanawake wa enzi zilizopita walizifahamu vizuri sana amri za Mungu kuhusu upatanisho kwa damu. Ilianza na Kaini na Abeli, ilithibitishwa na Nuhu (Mwanzo 9:1-6), ilidhibitiwa na sheria ya Agano la Kale, na ilikamilishwa na Yesu. Mungu alipoweka Sheria ya Musa, hakuanzisha dhabihu za wanyama kama ubunifu ambao haujawahi kuonekana na Waisraeli. Badala yake, aliwaonesha Waisraeli njia sahihi ya kutoa sadaka hizo, hadi wakati ambao dhabihu ya kumalizia ya Mwanawe itakapoleta mwisho wa haja ya dhabihu yoyote zaidi ya damu kupitia dhabihu za wanyama. Katika kuwaonesha njia sahihi, Mungu aliweka masharti madhubuti ili kuwaepusha watoto wa Israeli wasigeuzwe kuwa dhabihu zilizokubaliwa na Mungu hadi kutoa dhabihu watoto wao wasio na hatia kama vile wapagani waliowazunguka. Katika Mambo ya Walawi 18:21, Mungu aliwaambia watoto wa Israeli: “Wala usitoe yeyote kati ya uzao wako apite motoni kwa Moleki; wala usipate unajisi kwa jina la Mungu wako: Mimi ndimi Bwana.” Mungu alijitahidi kuwaonya Waisraeli dhidi ya kutoa watoto wao kama dhabihu kwa sababu ilikuwa inajulikana sana kuwa mataifa yaliyozunguka walishiriki katika mauaji kama hayo ya watoto. Swali linatokea, “Nini katika dunia hii kinaweza kumshawishi mama au baba kutoa watoto wao kwa mungu?” Hebu tuangalie jambo hili zaidi.
Wendy Davis anaandika kwa Widdershins, jarida linalojiita la uabudu usio na kipimo. Katika makala yake kwenye Mtandao wa Wavuti, As Old as the Moon: Sacrifice in History, alisema: “Kitendo cha mauaji ya ibada huenda ni cha zamani kama sisi [wanadamu—KB/BT] tulivyo.Katika enzi zote, watu walitoa sadaka walipohitaji kitu. Mababu zetu mara nyingi walitoa kitu bora zaidi walichokuwa nacho kwa mzaliwa wao wa kwanza, ili kujinusuru wenyewe” (1995, msisitizo umeongezwa). Umiliki wa thamani zaidi kwa mama au baba ulikuwa mtoto wao wa kwanza. Mtoto huyo, hata hivyo, alikuwa sio tu wa thamani, bali pia asiye na dhambi. Sadaka ya chochote chini ya kile kilicho safi na kisicho na dosari inapunguza thamani ya asili ya sadaka. Kwa hivyo, iliaminika kuwa sadaka safi na isiyo na dhambi ya kiwango kikubwa kama hicho ingeweza kuwaondolea wazazi dhambi (au, kwa jambo hilo, dhambi za kijiji kizima!). Kwa hivyo, dini zilizopotoka, na mbovu zilichipuka na kujihusisha na sadaka za watoto, mojawapo na maarufu zaidi ikiwa ni ya Moleki (angalia 2 Wafalme 23:10).
Lakini ingawa hata dhabihu ya watoto wachanga ilitimiza kipengele cha kutokuwa na dhambi kwa sadaka kamilifu,ilikuwa na mapungufu maeneo mengine. Kwa mfano, mtoto “wa kawaida” aliyezaliwa na wazazi maskini hakuwa sadaka yenye gharama kubwa zaidi inayopatikana; mtoto wa kifalme wa mfalme alikuwa bora zaidi. Kwa hiyo, kama Davis alivyobaini, hatimaye wafalme walitoa dhabihu watoto wao wenyewe ili kuwaridhisha “miungu.”
Lakini pia dhabihu ya mtoto wa mfalme bado haikuweza kuwakilisha dhabihu kamilifu, kwa sababu mtoto hakujitolea mwenyewe kwa hiari. Sadaka ya hiari ya damu ya kifalme ilikuwa karibu na sadaka kamilifu. Katika makala yenye kichwa No Greater Sacrifice, ambayo ilionekana kwenye Widdershins, mwandishi mmoja alipendekeza: “Sadaka ya hiari ni ya kuvutia zaidi. Kwa nini mtu anataka kujitoa muhanga kwa ajili ya kile wanachokiamini? Kwa kuangalia kihistoria, tunapaswa kuzingatia wafalme watakatifu ambao walijitoa muhanga kwa ajili ya Nchi” (angalia Andy, 1998). Ndiye, mfalme ambaye alijitolea kwa hiari yake mwenyewe ili awe karibu na dhabihu kamilifu. Shida pekee ya dhana kama hiyo ni kwamba, hakika hakuna mfalme aliyeishi maisha kamilifu. Kama mwandishi wa Widdershins alivyobaini kwa usahihi, katika jaribio la kutatua hili, “Hatimaye mtu alikuja na wazo la sadaka moja ya mwisho. Sadaka moja ya kuhesabu kwa wote waliobaki kwa wakati wote.Lakini nani angeweza kutolewa? Ilibidi iwe mtu muhimu sana; hata wafalme hawakuwa wazuri vya kutosha.Ni wazi kuwa, ni mungu tu aliyekuwa mkamilifu na mwenye kuhesabiwa kuwa wa mwisho” (Andy, 1998).
Kwa hivyo, kwa nini inasemekana wazi kuwa hata ulimwengu wa kipagani ulidai dhabihu ambayo haikuwa na dhambi,yaani ya kifalme, na ya hadhi ya juu kuliko wanadamu wengine. Doane alisema: “Imani ya ukombozi kutoka dhambini kwa mateso ya Uungu ulioingiliwa, iwe kwa kifo msalabani au vinginevyo, ilikuwa ya kawaida na maarufu miongoni mwa wapagani, karne nyingi kabla ya wakati wa Yesu wa Nazareti” (1882, ukurasa 183-185).
Mara tu tunapofahamu hitaji la kifo cha mungu-mwokozi, si vigumu kuona ni kwa nini wanadamu wangependa (na kuhitaji) kuona akishinda kifo. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania alizungumza kuhusu jambo hili aliposema kwamba Kristo alijitoa dhabihu ili “apate kuwaweka huru wale ambao kwa hofu ya mauti walikuwa katika utumwa maisha yao yote” (2:15). Kifo kinaogopesha zaidi kwa mwanadamu kuliko kitu kingine chochote duniani.Hii Ilikuwa kwa sababu ya kwamba, Wagiriki walimuumba Hercules nusu mwanadamu na nusu mungu—kushinda Ulimwengu wa Chini, na Wamisri walimfanya Osiris. Hakika mungu-mwokozi ambaye alijitolea kwa hiari yake kama sadaka kwa ajili ya wanadamu wote, angeweza kushinda adui mbaya wa wanadamu—Kifo. Kwa hivyo, wazo la mungu-mwokozi aliyetoa dhabihu ambaye anashinda kifo kwa ufufuo wake lilikuja kwa urahisi na kwa akili za watu waliokuwa wakijua kuwa wanahitaji msamaha,ambao walitaka sana kuishi baada ya kifo.
Na hivyo, kutoka kwa “mtazamo wa kiulimwengu,” makabila na dini mbalimbali—yakienea kwa maelfu ya miaka—yalibuni matoleo yao binafsi ya kile walichodhani kuwa mungu-mwokozi aliyefufuka anapaswa kuwa na kufanya. Wengine walisema alipasuliwa vipande kumi na vinne na kutawanywa kote nchini Misri (kwa mfano, Osiris). Wengine walisema angeonekana kama mwanadamu lakini angekuwa na nguvu za mwili zisizo za kawaida na kushuka kuzimu kumshinda Hadesi (kwa mfano, Hercules). Hata hivyo, jambo moja ni hakika: hadithi kuhusu shujaa aliyewaokoa wanadamu zilikuwa kwenye midomo ya karibu kila mpiga hadithi. Trench alisema kwa usahihi:
Hakuna mwanafunzi yeyote mwenye mawazo ya kina wa kumbukumbu za zamani za wanadamu anayeweza kukataa kutambua kwamba kupitia historia yote ya wanadamu kumekuwepo na matumaini ya ukombozi kutoka kwa uovu unaowakandamiza; na vile vile hawezi kukataa kwamba matumaini haya yamejishikiza mara kwa mara kwa mtu mmoja (ukuras 149).
Lakini inawezekanaje basi kudumisha kwamba mwokozi mmoja ambaye wanadamu wote walimngojea alikuwa, na ni, Yesu?
[Itaendelea]
MAREJELEO
Andy (1998), “No Greater Sacrifice,” Widdershins, 4[4]:no page number, [On-line], URL: http://www.widdershins.org/index.html.
Bales, James D. (no date), The Originality of Christ (Searcy, AR: Privately published by author).
Brown, Philip J. (2000), Dionysus [Online], URL: http://www.belinus.co.uk/mythology/Dionysus.htm.
Budge, E.A. Wallis, Trans. (1960), Papyrus of Ani: The Egyptian Book of the Dead (New York: Gramercy, 1999 reprint).
Butt, Kyle (2000), “The Historical Christ—Fact or Fiction,?” Reason & Revelation, 20:1-6, January.
Darrow, Clarence and Wallace Rice (1929), Infidels and Heretics: An Agnostic’s Anthology (Boston, MA: Stratford).
Davis, Wendy (1995), “As Old as the Moon: Sacrifice in History,” Widdershins, June 21, 1[2]:no page, [Online], URL: http://www.widdershins.org/index.html.
DeHoff, George W. (1944), Why We Believe the Bible (Murfreesboro, TN: DeHoff).
Doane, T.W. (1882), Bible Myths and Their Parallels in Other Religions (Kila, MT: Kessinger).
Encyclopaedia Britannica (1997), “Osiris” (London: Encyclopaedia Britannica, Inc.) 8:1026-1027.
Franklin, Stephen T. (1993), “Theological Foundations for the Uniqueness of Christ as Hope and Judge,” Evangelical Review of Theology, 17[1]:29-53, January.
Freke, Timothy and Peter Gandy (1999), The Jesus Mysteries (New York: Harmony Books).
Graves, Kersey (1875), The World’s Sixteen Crucified Saviors (Escondido, CA: The Book Tree, 1999 reprint).
Graves, Robert (1960), The Greek Myths (New York: Penguin).
Huxley, Julian (1960), “The Evolutionary Vision,” Issues in Evolution [Volume 3 of Evolution After Darwin], ed. Sol Tax (Chicago, IL: University of Chicago Press).
McCabe, Joseph (1993), The Myth of the Resurrection and Other Essays (Amherst, NY: Prometheus, reprint of 1926 edition).
Till, Farrell and Norman L. Geisler (1994), Debate held at Columbus College (Columbus, GA) on March 29. Quotations are from written transcript of the debate.
Trench, R.C. (no date), Christ the Desire of All Nations; or the Unconscious Prophecies of Heathendom, (Searcy, AR: Bales Publications).
Wilson, Edward O. (1978), On Human Nature (Cambridge, MA: Harvard University Press).
Woodward, Kenneth L. (2000), “The Other Jesus,” Newsweek, 135[13]:50-60, March 27.
Zomberg, Don (2000), “Letter to the Editor,” Newsweek, 135[16]:17, April 10.
Imechapishwa Februari 01, 2001
UZALISHAJI & MASHARTI: Tunayo furaha kutoa ruhusa ya makala hii kuzalishwa kwa sehemu au kwa ukamilifu, ili mradi masharti yetu yazingatiwe.
Masharti ya Uzalishaji→
REPRODUCTION & DISCLAIMERS: We are happy to grant permission for this article to be reproduced in part or in its entirety, as long as our stipulations are observed.