Menu
Glasses sitting on top of a Bible, with a large fingerprint in the foreground

Umuhimu wa Ushahidi katika Ukristo

Ijapokuwa “kina cha utajiri wa hekima na maarifa ya Mungu” ni ya kushangaza akili, na ingawa “hukumu Zake na njia Zake” haziwezi kuchunguzwa na “zimepita uwezo wa kuzitambua” (Warumi 11:33; Kumbukumbu la Torati 29:29), na hata ingawa binadamu wenye mipaka hawataweza kamwe kuelewa kikamilifu Muumba mtakatifu, asiye na mipaka, mwenye uweza wote, na mwenye kujua yote, hata hivyo, Mungu amekuwa akishughulika na wanadamu kwa njia za kimantiki akitoa ushahidi unaohitajika kwa ajili ya imani yenye mantiki. Fikiria, kwa mfano, jinsi Mungu amekuwa akihakikisha kuwa ushahidi wa kutosha unapatikana kwa wale wanaotafuta ukweli kwa uaminifu kujua kwamba Yeye yupo (rejea Mithali 8:17; Mathayo 7:7-8). Paulo aliandika: “Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu sifa Zake zisizoonekana zinaonekana wazi, zikifahamikwa kwa vitu vilivyoumbwa, yaani, uweza Wake wa milele na Uungu Wake, hata wasiwe na udhuru” (Warumi 1:20, msisitizo umeongezwa). Tangu wakati wa Adamu na Hawa, wanadamu wameweza kuona wazi jinsi “vitu vilivyoumbwa” vinavyoshuhudia kwa niaba ya Muumba mwenye nguvu, asiyeonekana. Kama vile mwandishi wa Zaburi alivyotangaza: “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga linaonyesha kazi za mikono Yake. Mchana husema na mchana, na usiku hufunua maarifa. Hakuna lugha wala maneno ambako sauti yao haisikiki. Uzi wao umeenea duniani pote, na maneno yao hadi mwisho wa ulimwengu” (Zaburi 19:1-4). Sababu kwa nini “mpumbavu amesema moyoni mwake, ‘Hakuna Mungu’” (Zaburi 14:1, msisitizo umeongezwa), ni kwa sababu Mungu amempa mwanadamu ushahidi wa kutosha wa kuwepo Kwake. Kwa bahati mbaya, mtu mpumbavu hukataa ushahidi huo.

Wakati nabii Samweli alipolihutubia taifa la Israeli katika sherehe ya kumtawaza Sauli, hakuja tu na hotuba ya hisia. Aliwaamuru, akisema, “Simameni tuli, ili niwahoji mbele za Bwana” (1 Samweli 12:7, msisitizo umeongezwa). Vivyo hivyo, Isaya aliandika: “‘Njooni sasa, nasi tuhojiane,’ asema Bwana, ‘Ijapokuwa dhambi zenu ni nyekundu kama damu, zitakuwa nyeupe kama theluji’” (Isaya 1:18, msisitizo umeongezwa). Fikiria pia tofauti kubwa kati ya Eliya na manabii wa Baali. Kwa matumaini ya kuvuta hisia za mungu wa uongo Baali, hawa manabii wa kujifanya waliokuwa na hisia kali “walirukaruka juu ya madhabahu,” “wakapaza sauti,” na “wakajikata kwa visu na mikuki, kama ilivyokuwa desturi yao, mpaka damu ikatoka kwa wingi” (1 Wafalme 18:26,28)— yote haya yalikuwa bure. Eliya, kwa upande mwingine, alikuwa na imani ya kimantiki iliyosimikwa katika Neno la Mungu. Alimwambia Mungu, “Nimefanya mambo haya yote kwa Neno Lako” (1 Wafalme 18:36, msisitizo umeongezwa). Imani yake binafsi, pamoja na ujumbe wa imani aliouhubiri, viliwekwa na kusimikwa katika Neno la Mungu Mwenyezi lililofunuliwa kwa njia ya kimantiki. Kwa maana, imani ya Kibiblia, hatimaye, “huja kwa kusikia, na kusikia kwa neno la Kristo” (Warumi 10:17).

Aina hii – hiyo ya imani na mahubiri yanayotegemea ushahidi wa kimantiki inaweza kupatikana katika Agano Jipya. Fikiria matendo na mafundisho ya Yesu. Angeweza tu kutangaza kwa ulimwengu kwamba Yeye ni Masihi. Angeweza tu kuwaambia watu kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu. Angeweza kutarajia kila mtu kuamini madai Yake kwamba alitumwa kutoka Mbinguni, na kamwe asingewapa watu wa wakati wake ushahidi wowote wa Uungu Wake. Hata hivyo, ingawa kulikuwa na nyakati ambapo Yesu alichagua kuto toa ushahidi wa ziada wa Uungu Wake (kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya wengi wa wasikilizaji Wake; kwa mfano, Marko 8:11-12), Yesu alielewa umuhimu wa ushahidi. Wakati wa huduma Yake duniani, aliwapa mara kwa mara ushahidi wa kutosha wa Uungu Wake. Alibainisha jinsi Yohana Mbatizaji alivyo toa ushahidi kwa niaba Yake (Yohana 5:33). Alisema, “Baba mwenyewe, aliyenituma, amenishuhudia” (Yohana 5:36, msisitizo umeongezwa; rejea Yohana 1:32-33; Mathayo 3:16-17). Alizungumzia jinsi “Maandiko…yanavyonishuhudia” (Yohana 5:39, msisitizo umeongezwa), na haswa alibainisha jinsi “Musa…aliandika kunihusu” (Yohana 5:46, msisitizo umeongezwa). Pia alibainisha jinsi kazi Zake za kimiujiza zilivyo toa ushahidi wa Uungu Wake (Yohana 5:36). Yesu alifanya miujiza mingi iliyodhihirisha nguvu Zake juu ya asili, magonjwa, mapepo, na kifo. Alielewa kwamba ushuhuda wake wa maneno peke yake usingemshawishi mtu yeyote katika mahakama ya sheria (Yohana 5:31; rejea Kumbukumbu la Torati 17:6; 19:15). Hivyo, katika Sikukuu ya Kutolewa Wakfu huko Yerusalemu aliwaambia Wayahudi wasioamini, “Kama sifanyi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini kama nazifanya, ijapokuwa hamniamini Mimi, ziaminini hizo kazi, mpate kujua na kufahamu ya kwamba Baba yu ndani Yangu, nami ni ndani Yake” (Yohana 10:37-38, msisitizo umeongezwa). Kwa bahati mbaya, maadui Wake wapumbavu na wakaidi walikataa mara kwa mara ushahidi usiopingika ambao Yesu aliwasilisha kwa niaba Yake.

Pengine ushahidi mkubwa zaidi ambao Yesu aliwasilisha kwa ajili ya Uungu Wake ulikuwa ufufuo Wake wa kimiujiza. Angeweza kufufuka kutoka kwa wafu na kutoonekana kwa mtu yeyote duniani. Angeweza kutoka kaburini na kuruhusu uvumi kuenea. Ukristo ungeweza kuanza kwa msingi wa kutoeleweka na ushirikina. Badala yake, Yesu alitangazwa kuwa Mwana wa Mungu… kwa ufufuo kutoka kwa wafu (Warumi 1:4). Alionekana akiwa hai kwa Maria Magdalena, kwa wale wanafunzi wawili waliokuwa njiani kuelekea Emau, kwa mitume, kwa Yakobo, na kwa zaidi ya wanafunzi 500 kwa mara moja, wengi wao wakiwa bado hai na wangeweza kuhojiwa miaka kadhaa baadaye wakati Paulo, ambaye pia alimshuhudia Mwokozi aliyefufuka, aliandika 1 Wakorintho (15:5-8). Yesu “aliudhihirisha uhai wake baada ya mateso yake kwa vielelezo vingi visivyoweza kukanushwa” (Matendo 1:3, msisitizo umeongezwa), kwa sababu Yeye ni Mkuu wa dini yenye mantiki. Msisimko, nguvu, na ujasiri ambao wanafunzi wa mwanzo walidhihirisha ulijengwa juu ya ushahidi thabiti wa ufufuo wa Yesu (miongoni mwa mambo mengine, kwa mfano, unabii uliotimizwa). Imani ya kimisheni, yenye nguvu, na yenye msisimko ya Wakristo wa karne ya 21 lazima vilevile iwe imejikita imara na kina katika ushahidi.

Yesu hakuwa ndiye pekee katika Agano Jipya aliyeonyesha umuhimu wa imani inayotegemea maarifa. Mathayo, Marko, Luka, na Yohana walijaza vitabu vyao vya injili na uthibitisho wa Yesu kuwa Kristo. Fikiria tu mwanzo wa vitabu hivi vinne. Mathayo alianza kitabu chake cha Injili kwa kuthibitisha kwa nasaba kwamba Yesu alikuwa uzao uliyoahidiwa wa Abrahamu na Daudi (Mathayo 1:1-17). Kisha alibainisha jinsi Yesu alivyokuwa amezaliwa na bikira, akitimiza unabii wa Isaya 7:14 (Mathayo 1:18-25). Marko alianza “injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu” (Marko 1:1) kwa kunukuu Malaki 3:1 na Isaya 40:3. Marko alithibitisha kiunabii kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa “sauti ya mtu aliaye nyikani,” na Yesu alikuwa “BWANA” (Marko 1:3). Luka pia alifungua kitabu chake cha kwa Habari Njema kwa kutegemea ushahidi, maarifa, na ufahamu.

Kwa kuwa wengi wamejitahidi kupanga simulizi ya mambo yale yaliyotimizwa kati yetu, kama vile walivyotueleza wale waliokuwa mashahidi wenyewe tangu mwanzo na wahudumu wa neno, nami pia niliona ni vema, kwa kuwa nimepata ufahamu kamili wa mambo yote tangu mwanzo, kukuandikia wewe mfuatano wa mambo hayo, ewe Theofilo mtukufu, ili ujue hakika ya mambo yale uliyofundishwa (Luka 1:1-4).

Kisha tuna kitabu chake cha injili ya Yohana, ambacho, kutoka mwanzo hadi mwisho, imejaa uthibitisho kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu anayefanya miujiza (1:3; 2:1-11; 20:30-31; 21:25). Kwa kweli, lengo lililotajwa la kitabu chake ni miujiza mbalimbali ya Kristo (na kulikuwa na miujiza mingine mingi ambayo Yohana hakuitaja) ilikuwa ili “muamini kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini, mpate kuwa na uzima kwa jina lake” (20:30-31). Ikiwa imani ya Kibiblia ni tu “imani thabiti katika jambo ambalo hakuna ushahidi,” ambayo ni mojawapo ya ufafanuzi ambao Merriam-Webster (mtandaoni) unatoa kwa neno “imani” (2011), basi kwa nini Yohana na waandishi wa sinoptiki walitumia muda mwingi kutoa ushahidi kuhusu ni nani Yesu? Jibu: Kwa sababu ukweli wa Mungu, Neno lake, na Mwana wake ndio msingi wa imani ya kweli (Yohana 8:31-32; 17:17; Warumi 10:17).

Wakati mtume Paulo aliposimama mbele ya Festo na Mfalme Agripa, alizungumzia mambo hayo “ambayo manabii na Musa walitabiri kwamba yangetokea—ya kwamba Kristo angepaswa kuteseka, kwamba angekuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, na angehubiri mwanga kwa watu Wayahudi na watu wa Mataifa” (Matendo 26:23-24). Hata hivyo, wakati Paulo “alipofanya utetezi wake, Festo akasema kwa sauti kubwa, ‘Paulo, wewe umechanganyikiwa na elimu nyingi inakufanya uwe mwenda wazimu!’” (26:24). Paulo alijibu vipi? Je, aliitikia kwa ombi la hisia tu? Je, alikaribisha wazo la Injili isiyo na mantiki, isiyo thibitishika? Hata kidogo. Paulo kwa unyenyekevu, lakini kwa ujasiri, alijibu: “Si kwa kuwa mimi nimepoteza akili, mkuu Festo, lakini nasema maneno ya kweli na ya akili” (Matendo 26:25).

HITIMISHO

Kwa kusikitika, wengi kati ya watu wenye uwezo wa kuwajibika duniani hawataikubali mlima wa ushahidi wa Ukristo na kuwa Wakristo (Mathayo 7:13-14). Lakini sisi ambao tunachagua kuweka imani yetu katika Mungu, Yesu, na Neno lake, tunaweza kufanya hivyo kwa sababu “ukweli” unaweza kujulikana (Yohana 8:32), kufuatwa kwa haki (Warumi 6:17; 10:12-13), na kulindwa kwa mantiki (1 Petro 3:15).


Published

A copied sheet of paper

REPRODUCTION & DISCLAIMERS: We are happy to grant permission for this article to be reproduced in part or in its entirety, as long as our stipulations are observed.

Reproduction Stipulations→