Ubatizo na Mlinzi wa Gereza wa Filipi
Wengi miongoni mwa Wakristo wameamua kwamba ubatizo wa maji hauhitajiki na wala sio wa lazima kwa wokovu. Wakiwa wameshawishiwa kwa kiasi kikubwa na Wanamageuzi wa ki-protestanti, watu wameshawishika kwamba msamaha wa dhambi kwa damu ya Kristo unapatikana, pale mtu “anapoamini” – kwa hilo wanamaanisha kwamba, pale mu anapoamua kwa hiari yake kumkubali Kristo kama Bwana na mwokozi. Kwa wao, tendo la nje, la ubatizo wa maji, unachukuliw kiurahisi kama ishara ya nje au beji ambayo inathibitisha wokovu wa Mkristo, ambao umeshapatikana. Aya moja ambayo huwa inatumika kuunga mkono wazo hili, ni mazungumzo ya Bwana jela kule Filipi (Matendo 16). Hata hivyo tafakari ya kina ya kile kisa inatoa hitimisho tofauti kabisa.
Pale tetemeko lilipo “rocked” ile Jela, ambamo Paulo na Sila walikuwa wamefungwa, bwana Jela alidhani wafungwa wametoroka. Hii ni kutokana na ukweli kwamba sheria ya Kirumi ingehitaji maisha yake, kama adhabu ya kumpoteza mfungwa aliye chini ya uangalizi wake (Angalia Ramsay 187, Uk 222; akinukuu Matendo 12: 19), alichomoa upanga wake, akitaka kujiua, lakini Paulo aliita kwa sauti, akimtaka mlinzi wa gereza, asijidhuru, akimhakikishia kwamba hakuna mfungwa aliyetoroka. Akawasha taa na kwenda gerezani, akaanguka chini akitetemeka mbele ya kina Paulo na Sila. Akawatoa nje ya gereza, mlinzi yule akawauliza Paulo na Sila, “Mabwana zangu” yanipasa nifanye nini, ili nipate kuokoka? (Matendo 16: 30).
Huyu mlinzi alimaanisha nini kwa kauli hii? Kama mpagani wa ki-Rumi (rejea Alford, 1980, 2: 184), alikuwa bila shaka anafahamu simulizi za ki-Rumi au ki-Giriki kwa maisha yake yote. Ukristo ulianzishwa Makedonia, siku chache tu kabla, pale Paulo alipofika Filipi (Matendo 16: 12, rejea Ramsay, Uk 215). Kwa hiyo, pasipo shaka alikuwa na uelewa wa kutosha juu ya wazo la kikristo la wokovu toka dhambini. Lakini matukio yaliyotokea siku zile na kupelekea wokovu wake, yanaweza kuwa ndiyo chanzo cha swali la mlinzi yule.
Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na Pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida kubwa kwa kuagua. Binti huyu, Kijakazi, akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele akisema, “watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria watu njia ya wokovu”. Akafanya hayo siku nyingi (Matendo 16: 16-18).
Angalia kwamba, yule Pepo ndani ya yule binti, alitangazia raia wa Filipi, kwa kipindi cha “siku nyingi” ukweli kwamba Paulo na Sila, walikuwa ni wawakilishi wa Mungu pekee wa kweli, na kwamba walikuwa na habari ambazo zingewaonyesha watu njia ya wokovu. Inawezekana huyu mlinzi alisikia tangazo hili, au moja kwa moja au kwa kuambiwa na marafiki, jirani zake, ndugu na hata watu wa mjini.
Baadaye baada ya Paulo kumtoa yule Pepo toka kwa binti yule, bwana zake wakawakamata Paulo na Sila, na kuwakokota mpaka sokoni, mbele ya wakuu wa mji, wakawashitaki na hatimaye wakajikuta gerezani, walipokutana na mlinzi. Inawezekana sana kwamba mlinzi huyu alijua mashitaka haya, ambayo kwa kweli yaliwaelezea wao kama “watumishi wa Mungu aliye juu” ambao pia wanayo habari inayohusu “njia ya wokovu”
Njia ya tatu, ambayo kwayo inawezekana mlinzi huyu alikuwa na taarifa za kutosha zilizopelekea kuuliza lile swali, inaweza kuonekana katika mstari wa 25, “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza”. Yawezekana huyu mlinzi pia alisikiliza nyimbo walizoimba Paulo na Sila, ambazo huenda ziliongelea Mungu, Kristo na Wokovu.
Mazingira haya matatu, yanaweza yakawa yamesababisha ombi la mlinzi kujulishwa habari ya wokovu – hata hivyo uelewa wake lazima ulikuwa hatua kwa hatua. Jibu la Paulo kwa swali la mlinzi ni “mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na nyumba yako” (Mstari wa 31). Paulo alimaanisha nini kwa kauli hii? Kama alimaanisha kile ambacho Madhehebu ya Kikristo wanadhani, kwamba, kama mlinzi tayari alijua Bwana Yesu ni nani, na kama Paulo alikuwa anamsihi kuamini tu (yaani kumkubali Kristo ndani ya Moyo wake kama mwokozi wake), basi tutegemee aya hiyo kutoa jibu au kauli ya bwana Jela – Kwamba alimpokea Yesu Kristo kama mwokozi wake, au kwamba alimwamini Bwana Yesu palepale, na akawa ameokolewa.
Lakini kinyume chake, aya inasema “wakamwambia neno la Bwana” (Mstari wa 32). Kwa nini? Je Paulo hakufanya hivyo kwa kumwambia mlinzi huyo wa gereza kuamini tu? Kwa kweli hapana! Paulo baadaye aliandika kwamba “imani huja kwa kusikia … neno la Bwana” (Warumi 10: 17). Na kwa hiyo bwana Jela huyo alihitaji kusikia habari zaidi, ambazo zingemuwezesha kujua nini maana ya kumwamini Yesu. Kinachofuata sasa ni kwamba, yale maelekezo aliyopewa “Mwamini Bwana Yesu Kristo” kimsingi ilikuwa ni kauli inayoenda mbali, ikikusudia kuelekeza upya mshikamano wa bwana jela na imani zile za miungu ya kipagani ya Wagiriki au Warumi, kuelekeza kwa mtu anayestahili kuaminiwa – Yesu Kristo. Ilikuwa ni namna ya kupangilia upya fikra za bwana Jela kumuelekea Yesu Kristo na sio zile imani za kipagani tena. Lakini kama wangemwambia bwana Jela (au mtu mwingine yeyote leo) “Kumwamini Bwana Yesu” hakutoi taarifa za kutosha za namna ya kuamini. Kwa maneno mengine, kuna zaidi ya “kumwamini Bwana Yesu” na sio tu kukiri akilini mwako kwamba Yesu Kristo ni Bwana na Mwakozi (ukweli ambao hata Shetani na Mapepo wanaujua – Mwanzo 3: 15; Mathayo 4: 3, 6; Luka 22: 31; waebrania 2: 14; Yakobo 2: 19; Ufunuo 12: 4… ).
Ilikuwa ni katika kusema neno la Bwana kwa mlinzi wa gereza, kwamba alielewa Kristo ni nani, na Ukristo unahusu nini, na utii sahihi wa neno lililohubiriwa – yaani walimaanisha nini kusema “Mwamini Bwana Yesu”. Kwa kuwa mlinzi yule asingeokolewa kabla Paulo hajamwambia neno la Bwana. Angalia mtiririko huu wa matukio, ambayo aya hii inatueleza, mara tu baada ya kuelezwa neno la Bwana;
- Mlinzi wa gereza aliwachukua Paulo na Sila “saa ileile ya usiku na kuwaosha mapigo” (Matendo 16: 33). Huu ni ushahidi wa toba, (mfano wa Mathayo 3: 8). Huu ni ushahidi kwamba mlinzi huyu alishawishika kwa zile taarifa alizopewa, kwa kiwango kwamba alitaka kusahihisha makosa. Hii ni toba, kubadilika kwa fikra, kunakopelekea matendo ya nje yaliyo sahihi (Mathayo 21: 29; I Wakorintho 7: 10).
- Aya ile inaendelea kusema “kisha akabatizwa yeye na watu wake wote wakati huo huo” kuna namna tatu ya kuangalia kauli hii; kama ubatizo haukuwa kitu cha lazima kwenye wokovu, kwa nini kinatajwa hapa kwenye mazungumzo na bwana Jela? Kwa nini wasingeendelea kuelezea kilichotokea baada ya mazungumzo – yaani baadhi ya vielelezo kwamba tayari alikuwa ameshaokolewa? Kama ubatizo sio kitu cha lazima, badala ya kusomeka “na kisha yeye na familia yake walimpokea Yesu kama Mwokozi wao”. Pili; Huyu mlinzi wa gereza alipata wapi wazo kwamba anatakiwa kubatizwa? Itakuwa alisikia katika “kumwambia neno la Bwana” kulikofanywa na Paulo. Na kama Paulo lilijumuisha hili la ubatizo katika “kumwambia neno la Bwana” kinachofuata ni kuwa, wokovu wa mlinzi wa gereza ulitegemea kwa kiasi ubatizo. Tatu; kwa nini alibatizwa mara tu? Wengi katika madhehebu ya kikristo, wanasubiri wiki nzima, au mwezi, au zaidi kabla hawajabatiza waumini wao, kwa nini mlinzi wa gereza alibatizwa mara tu tena katikati ya usiku? Hii inaashiria kwamba ubatizo ni jambo la lazima na la haraka kuliko wengi wanavyodhania leo.
- Mpaka wakati huu, kwa maelezo ya Luka, tunaambiwa kwamba huyu mlinzi aliwaleta Paulo na Sila nyumbani kwake, na kuandaa chakula mbele yao. Halafu tunaambiwa kwamba huyu mlinzi wa gereza “akafurahi” (Mstari 34). Ni wakati gani aya hii inaonyesha kwamba huyu mlinzi alionyesha ishara ya furaha na raha (ambavyo hufuatana na mazungumzo) – Kabla au Baada ya ubatizo? Ni baada ya Ubatizo! Na ki-ukweli, kila mara furaha inatajwa wazi katika mazungumzo ndani ya kitabu cha Matendo, mara kwa mara huwa ni baada ya Ubatizo (Angalia 2: 46 “kwa furaha”; na 8: 39 “akifurahi”).
- Kila kitu mpaka wakati huu kinamuongoza mtu katika hitimisho moja tu, kwamba Ubatizo ulikuwa ni sehemu muhimu wa kuokolewa kwa mlinzi wa gereza, na ulitangulia wokovu wake kama tendo lililoukamilisha. Huu ni ukweli hasa; angalia vizuri kauli hii katika mstari wa 34; “maana amekwisha kumwamini Mungu” Hii ni ishara pekee (explicit) na ya wazi kwamba, mlinzi sasa alikuwa ni muumini aliyeokolewa. Katika Kigiriki, kauli hii, “maana amekwisha kumwamini” (pepisteukos) ni wakati ulio kamili. Hakuna wakati kama huo katika Kiingereza. Zingatia maelezo yafuatayo, yaliyotolewa na watalam wa Kigiriki Dana na Mantey.
Wakati ulio kamili, unawakilisha tendo lililokamilika. Umuhimu wake hasa ni ule mwendelezo wa tendo au hali ya kumalizika na kuwepo kwa matokeo yake yaliyokamilika. Yaani kwamba, unaliona tendo kama zao lililokamilika … Ikimaanisha mchakato, lakini ikiona kama umefikia utimilifu wake na uko katika hali iliyokamilika (1927, Uk 200 pamoja na fafanuzi).
Msomi wa Kigiriki Ray Summers alitoa maelezo mengine yaliyosaidia sana kuhusu wakati uliokamilika katika Kigiriki;
Unaonyesha tendo lililokamilika pamoja na matokeo ya kuwepo. Sisitizo la msingi ni juu ya matokeo ya ile hali ya kuwepo. Mawazo matatu yanajumuishwa katika wakati huu uliokamili; Tendo linaloendelea, linapokuja kumalizika, jinsi lilivyo katika ukamilifu wake. Hii inamaanisha mchakato, lakini ukiangalia kama umefikia utimilifu, na jinsi ulivyo katika ukamilifu wake (1950, Uk 103, pamoja na fafanuzi).
Tukiangazia msukumo huu wa wakati ulio kamili katika Kigiriki, Luka alikuwa akikazia kwamba mlinzi yule alipitia katika mchakato wenye matendo mengi, kabla haijasemekana kwamba alikuwa na imani inayookoa katika Bwana. Imani yake ya mwanzo, iliyokuja kama matokeo ya kusikia neno la Bwana likihubiriwa kwake lilipelekea toba yake (kama ilivyothibitishwa na kuhudumia vidonda vya Paulo na Sila), na likamalizikia katika ubatizo wake katika maji – na hivyo kuleta imani yake katika ukamilifu. Ni katika wakati huu tu, ambapo wakati ulio kamili katika Kigiriki, unaweza kutumika kuonyesha kwamba mlinzi yule sasa, anasimama katika hali ya ukamilifu kwamba ameamini. Lua alikuwa makini kujitoa katika kumuonyesha kama ameamini, mpaka matakwa yote ya wokovu yawe yamekamilika, na hivyo kupelekea imani kwenye ukamilifu. Uchunguzi huu ulitambuliwa na R. J. Knowling, akiwa ni Profesa wa Agano Jipya, katika Chuo cha Mfalme, huko London. “Neno pepisteukos, linaonyesha kwamba ukamilifu huu wa furaha, ulisababishwa na ukiri ulio kamili wa imani; ilikuwa ni furaha ya roho mtakatifu iliyofuatia ubatizo wake” (2: 353 pamoja na fafanuzi).
Uelewa huu wa mazungumzo ya mlinzi wa gereza huko Filipi unaendana kabisa na mazungumzo mengine katika kitabu cha Matendo (mfano; Matendo 2: 38; 3: 19; 8: 12-13, 36 – 39; 9: 18; 10: 47 – 48; 16: 15; 18: 8; NA 19: 5). Agano Jipya, linaonyesha kuzamisha katika maji kama ni wakati ambapo Mungu anasafisha roho iliyochafuliwa na dhambi, ya yule anayeamini kwa damu ya Yesu Kristo (Angalia Matendo 22: 16; Warumi 6: 3-4).
Rejea
Dana H E and Julius Mantey (1972), A Manual Grammer of the Greek New Testament.
Knowling R. J (No Date), The Expositor’s Greek Testament: The Acts of the Apostles
Ramsay, William (1897) St. Paul the Traveller and the Roman Citizen
Summers Ray (1950), Essentials of New Testament Greek.
Ilichapishwa, Septemba 30; 2004.
REPRODUCTION & DISCLAIMERS: We are happy to grant permission for this article to be reproduced in part or in its entirety, as long as our stipulations are observed.