Menu

Kwanini Ilipaswa Yesu Afe?

Swali:
Ikiwa Mungu ni wa upendo na mwenye nguvu zote, kwa nini Yesu ilibidi afe ili Mungu aweze kusamehe dhambi?

Jibu:
Biblia inafunua kuwa Mungu ni wa upendo na mwenye nguvu zote, lakini Yeye si wa upendo na mwenye nguvu zote tu. Hiyo ni kusema, Mungu si Kiumbe aliye na sifa moja au mbili tu. Mungu ni mkamilifu katika sifa Zake zote, ikiwa ni pamoja na utakatifu Wake. Mungu ni safi na mtakatifu asilimia 100. Yeye ni mtakatifu katika maana kamilifu. “Bwana ni mnyofu;… hakuna udhalimu ndani Yake” (Zaburi 92:15). “Mungu ni nuru, na ndani Yake hamna giza hata kidogo” (1 Yohana 1:5). Mwandishi wa zaburi alimtukuza Mungu akisema: “Hakuna uovu unaokaa nawe” (5:4, NASB). Hakuna chembe ya dhambi inayoweza kukaa ndani ya Mungu au pamoja na Mungu kwa sababu hata kiasi kidogo cha uovu kinapingana na asili Yake safi na takatifu. Hakika,“Bwana Mungu Mwenyezi” ni “mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu” (Ufunuo 4:8; Isaya 6:3).¹

Mbali na asili ya Mungu iliyo takatifu kabisa ni asili Yake ya haki isiyo na mipaka. “Kazi yake ni kamilifu; kwa maana njia Zake zote ni za haki, Mungu wa kweli na asiye na udhalimu; mwenye haki na mnyofu ndiye” (Kumbukumbu la Torati 32:4). Mwandishi wa zaburi alimwambia Mungu: “Haki na hukumu ndizo msingi wa kiti Chako cha enzi” (89:14). Tofauti na majaji wa dunia ambao mara nyingi hukosa katika utekelezaji wa haki, Mungu “haoneshi upendeleo wala hapokei rushwa” (Kumbukumbu la Torati 10:17). Jaji fisadi huruhusu wenye hatia kutopewa adhabu, wakati jaji mwenye haki hutoa hukumu ya haki kwa wavunja sheria (linganisha Wakolosai 3:25).

Utakatifu kamilifu wa Mungu hufanya ushirika na uovu kuwa kitu kisichowezekana kabisa. Haki kamilifu ya Mungu inahitaji adhabu kwa kila tendo la uovu. Dhambi ni mbaya sana mbele za Mungu kiasi kwamba adhabu ya kuvunja sheria Yake ni kifo—kutengwa milele na Yeye (Warumi 6:23; 1 Yohana 3:4). Kila mwanadamu mwenye akili timamu kwa wakati fulani humtenda Mungu dhambi (Warumi 3:10, 23). Tunatenda dhambi na hivyo tunajitenga na Muumba wetu mtakatifu. Tunajikuta (kwa matendo yetu wenyewe) “tumekufa kwa makosa na dhambi” (Waefeso 2:1). Tumepotea katika dhambi, “tukiwa hatuna tumaini na bila Mungu” (Waefeso 2:12). Na, kama wenye dhambi, hatuna uwezo wa kujinusuru wenyewe. Hakuna kitu tunachoweza kufanya. Hakuna mpango tunaoweza kuunda ili kuepuka adhabu kutoka kwa Mungu mwenye utakatifu na haki kamilifu. Gharama lazima ilipwe kwa dhambi.

Hii ndiyo sababu ya Yesu kuja duniani. Hakulazimishwa; alichagua. Alikuja ili kutosheleza utakatifu na haki kamilifu ya Mungu (ambayo ni utakatifu na haki Yake mwenyewe). “Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu” (1 Wakorintho 15:3). Alijitolea kwa hiari Yake kulipa gharama ya juu kabisa kwa ajili ya dhambi zetu, akionesha kuwa Mungu si mtakatifu na mwenye haki tu; Yeye ni upendo (1 Yohana 4:8)! Na, “Hakuna upendo mwingi zaidi ya huu, yaani mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yohana 15:13).

Upendo kamilifu wa Mungu ulimlazimisha Yesu kubeba adhabu yetu juu Yake. “Mungu, aliye mwingi wa rehema, kwa ajili ya upendo wake mkuu aliotupenda, hata tulipokuwa wafu kwa makosa yetu, alituhuisha pamoja na Kristo (kwa neema mmeokolewa)…. [N]a katika Kristo Yesu ninyi mliokuwa mbali mmekaribiwa kwa damu ya Kristo” (Waefeso 2:4-5, 13). “Kwa maana Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16).

Utakatifu kamilifu na haki ya Mungu vinahitaji kwamba “mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23). Lakini shukrani kwa Mungu, huo si mwisho wa hadithi! (Angalau haipaswi kuwa.) Warumi 6:23 inasema nini baadaye? “Bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Ndiyo, Mungu ni “mwenye haki” na “anayewafanya wanadamu kuwa waadilifu”² kupitia jibu pekee na lisilo na dhambi la tatizo la dhambi—Yesu Kristo (Waebrania 4:15), Ambaye kusudi lake pekee la kuja duniani lilikuwa ni kuokoa nafsi za wanadamu wenye dhambi (Mathayo 1:21; Luka 19:10).

Jambo lisilo na mantiki, lenye kuvunja moyo, na baya zaidi ambalo mwanadamu aliyeangamia katika dhambi anaweza kufanya ni kukataa mwaliko wa Mungu wenye upendo wa kukubali karama ya bure ya wokovu wa milele kupitia Yesu.³ Kwa upande mwingine, mambo mawili makubwa zaidi tunayoweza kufanya katika maisha yetu ya kimwili ni (1) kumkubali na kumfuata Yesu, Ambaye ni “njia, na kweli, na uzima” (Yohana 14:6); na (2) kuwaambia wengine juu ya kwa nini Mwokozi wetu alikuja duniani (Mathayo 28:18-20; Matendo 8:4; Warumi 1:16).

TANBIHI ZA MWISHO

1 Asili ya Mungu ya uweza wa milele (uwezo wote) haipingani na utakatifu Wake kwa kuwa uweza wa Mungu haumaanishi kwamba Anaweza kufanya kila kitu na chochote. Maandiko yanaweka wazi, kwa mfano, kwamba Mungu “hawezi kusema uongo” (Tito 1:2; Waebrania 6:18). Kwa hivyo, mafundisho ya Biblia kuhusu uweza wa Mungu ni kwamba Anaweza kufanya chochote (1) ambacho kinawezekana kimantiki kufanyika (mfano, Hawezi kuumba mduara wenye pembe nne), na (2) ambacho kinaendana na mapenzi Yake matakatifu. [Kwa maelezo zaidi, tazama Dave Miller.(2009), “Things God Cannot Do,” https://apologeticspress.org/things-god-cannot-do-1240/.]

2 Kupitia imani ya kweli na ya kibiblia kwa Yesu, Mungu alitufanya kuwa “wenye haki” mbele za Mungu ambaye ni mwenye haki kamilifu (Warumi 3:26).

3 Kujifunza zaidi kuhusu kupokea zawadi ya wokovu na kuwa mfuasi wa Kristo, angalia kijitabu cha bure cha AP kwenye. https://apologeticspress.org/wp-content/uploads/2021/08/Receiving-the-Gift-of-Salvation.pdf.


Published

A copied sheet of paper

REPRODUCTION & DISCLAIMERS: We are happy to grant permission for this article to be reproduced in part or in its entirety, as long as our stipulations are observed.

Reproduction Stipulations→