Je, Ni Muujiza?
Mtu hawezi kusoma kurasa nyingi kutoka kwenye Agano Jipya (au Agano la Kale) bila kukutana na muujiza. Miujiza imetapakaa kwenye kurasa za Biblia kama madoa kwenye mbwa Dalmatian: mapigo 10 huko Misri; uponyaji wa watu wenye ukoma; kufufuka kwa wafu; kuzaliwa kwa bikira; n.k. Hata hivyo, watu wengi walioelimika wanakanusha wazo kwamba miujiza ilikuwa halisi au inawezekana. Badala yake wanasisitiza kuwa maajabu yaliyoandikwa kwenye Biblia lazima yalikuwa ya kubuni au yalikuwa na maelezo ya asili tu. Je, Yesu na wengine katika Biblia walifanya miujiza mikubwa au ni hadithi tu za “kuwaza tu”, kwa watu wenye imani za kijinga na wasio na sayansi?
MUUJIZA NI NINI?
Ili kuamua kama miujiza ilitokea kweli, kwanza tunapaswa kuelewa maana ya muujiza. Muujiza ni tukio linalokiuka sheria za asili na ambalo linaweza kuelezeka tu kwa maelezo ya kiroho. Kwa mfano, kutembea barabarani si muujiza. Lakini kukiuka sheria ya mvuto na kutembea juu ya maji ni muujiza. Hakuna kitu cha kushangaza kuhusu kumfufua mtu kwa kutumia CPR. Lakini kuna kitu cha kimuujiza kuhusu kumfufua mtu aliyekufa kwa siku kadhaa.
WENGINE WANASEMA “HAKUNA” MIUJIZA
Baadhi ya watu wanasisitiza kwamba aina yoyote ya muujiza haiwezekani kabisa.Kwa nini wanasema “hakuna” miujiza? Kuna sababu nyingi lakini labda muhimu zaidi ni kwamba hawana imani kuwa Mungu yupo (au kwamba kama yupo hawezi kuingilia kati, katika ulimwengu wa asili). Mtu anayeamini kwamba Ulimwengu na maudhui yake yamekuwepo kupitia michakato ya asili kwa mabilioni ya miaka, hawezi kuamini miujiza kwa sababu anaamini kwamba hakuna kitu kinachopatikana nje ya asili. Kama alivyosema mnajimu mashuhuri kutoka Chuo Kikuu cha Cornell Carl Sagan: “Anga ndilo pekee lililopo au lililowahi kuwepo au litakalokuwepo” (1980 ukurasa 4). Kwa kuwa muujiza ni tukio lenye maelezo ya kiroho, hakuna tukio kama hilo linaloweza kutokea katika ulimwengu ambapo nguvu za asili tu ndizo zinazoliendesha. Mara mtu anapokataa muujiza mkubwa zaidi ya yote–kwa vilivyoumbwa mikononi mwa Mungu – basi yeye analazimika kukataa kwamba miujiza ya aina yoyote inaweza kutokea.
Wale wanaoshikilia mtazamo huo wako sawa kuhusu jambo moja: Ikiwa Mungu hayupo (au kama yupo lakini hayuko tayari kuingilia kati katika uumbaji wake) basi miujiza haiwezi kutokea. Kwa upande mwingine, ikiwa Mungu yupo (na inawezekana kusemwa kwa ushawishi kwamba yupo!) basi miujiza siyo tu kwamba inawezekana bali pia inatarajiwa. Ina maana nzuri kabisa kuhitimisha kwamba ikiwa Mungu aliumba Ulimwengu huu basi mara kwa mara Anaweza kuingilia kati kupitia miujiza ili kutimiza malengo yake ya kimungu.
MUNGU ASINGEVUNJA SHERIA, AU SIO?
Wazo jingine linapendekeza kwamba Mungu aliumba Ulimwengu lakini shughuli zake ziliishia kwenye uumbaji. Baada ya hapo Hakuingilia kati tena katika ulimwengu huu kupitia miujiza, kwa kufanya hiyo ingekuwa kuvunja sheria za asili ambazo Aliweka wakati wa uumbaji.
Tatizo la wazo hili ni kwamba halizingatii ukweli kwamba sheria za asili hazimuhusu Mungu (kwa kuwa yeye si Kiumbe “wa asili”). Sheria za asili haziwezi kuvunjwa. Kwa mfano, Sheria ya Kwanza ya Mabadiliko ya Joto inaeleza kwamba: Kani au nishati haiwezi kutengenezwa au kuharibiwa katika asili. Maneno mawili “katika asili” lazima yajumuishwe kwa sheria kuandikwa kwa usahihi. Hakuna kitu katika asili – binadamu, wanyama au kitu – kinachoweza kuvunja sheria hii. Hata hivyo, kwa kuwa Mungu si sehemu ya asili, sheria hii haina maana kwake.
Ili kufafanua, fikiria Ulimwengu kama chumba kimoja. Mungu aliweka sheria za asili zinazohusu kila kitu katika chumba hicho kisha akafunga mlango. Haiwezekani kwa Kani au nishati kuundwa au kuharibiwa katika chumba hicho. Lakini fikiria kama Mungu akifungua mlango na kuweka kiti kingine ndani ya chumba au kutoa kiti kutoka chumbani. Je, Mungu atakuwa amevunja sheria aliyoiweka katika chumba hicho? Hapana, kwa sababu kila kitu ndani ya chumba (Ulimwengu) kinaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za asili lakini kwa kuwa Mungu yupo nje ya chumba basi sheria zinazofanya kazi ndani ya chumba hazimuhusu Yeye.
Miujiza haiwezekani tu katika ulimwengu usio na Mungu au Mungu asiyeingilia kati. Mara uwepo wa Mungu na uwezo wake wa kufanya kazi katika ulimwengu wa asili unapothibitishwa, ina maana nzuri kabisa kuhitimisha kwamba Anaweza kufanya mambo ya kiroho mara kwa mara ili kutimiza malengo Yake. Mungu si mwizi wa ulimwengu anayezunguka “akihitaji kuvunja sheria” za asili. Badala yake ni Muumba mwenye enzi ambaye ana haki ya kufanya kazi wakati wowote na kwa njia yoyote aonavyo inafaa.
MAREJELEO
Sagan Carl (1980) Cosmos (New York: Random House).
UZALISHAJI & MASHARTI: Tunayo furaha kutoa ruhusa ya makala hii kuzalishwa kwa sehemu au kwa ukamilifu, ili mradi masharti yetu yazingatiwe.
REPRODUCTION & DISCLAIMERS: We are happy to grant permission for this article to be reproduced in part or in its entirety, as long as our stipulations are observed.