Je, Kunyunyiza ni Njia Inayofaa kwa Ubatizo?
Katika tafsiri zao za “ubatizo,” kamusi nyingi za kisasa zinajumuisha kunyunyiza (na kumimina) maji. Vile vile, wengi katika ulimwengu wa kidini hufundisha kwamba “ubatizo” kwa kunyunyiza unakubalika na unatosha, wakati wengine hawakubaliani. Kutokana na ujumbe huu unaokinzana, maswali juu ya suala la kunyunyiza hayakwepeki. Neno “ubatizo” lina maana gani hasa? Je, linaweza kumaanisha kunyunyiza? Majibu ya maswali haya yana athari kwa maana ya amri ya Yesu, “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu …” (Mathayo 28:19, imesistizwa).
Neno la Kiingereza “baptism” linatoka kwenye neno la Kigiriki baptisma, ambalo lina maana ya kuzamisha au kuloweka (Thayer, 1958, ukurasa 94; Arndt, Gingrich, na Danker, 1979, uk. 132). Kuzamisha na kunyunyiza ni mambo mawili tofauti sana, na lugha ya Kigiriki inaonesha tofauti hiyo (Jackson, 2002a, uk. 31). Matumizi ya neno baptisma yanapatikana katika maandiko mbalimbali ya Kigiriki yasiyo ya kibiblia, ambapo kila mara yanamaanisha kuzamisha. Aristotle, Polybius, Plutarch, Strabo, Diodorus, na Josephus wote waliandika kuhusu vitu vilivyokuwa “vimezamishwa” kwenye maji, na walitumia aina mbalimbali za neno baptizo (Martin, 1991, ukurasa 208-210). Katika toleo la Kigiriki la Agano la Kale, Septuagint, kuna kifungu ambacho kinadhihirisha wazi tofauti kati ya dhana ya kunyunyiza na ubatizo. Mambo ya Walawi 4:17 inasomeka: “Kisha kuhani atachovya [baptizo] kidole chake katika damu, na kunyunyiza [rhantizo] mbele ya Bwana, mbele ya pazia.” Katika aya hii, neno lililotafsiriwa “kubatiza” (au “kuchovya”) limetajwa katika sentensi moja na neno lililotafsiriwa kwa usahihi “kunyunyiza,” kwa hivyo ni wazi kwamba katika Agano la Kale, kunyunyiza si ubatizo. Hali hiyo inashikilia ukweli katika Agano Jipya. Katika Yohana 13:16, Yesu “alichovya” (Kigiriki bapto) kipande cha mkate na kumpa Yuda. Kila mara “ubatizo” unapotajwa katika Agano Jipya, maana yake ni kuzamishwa, sio kunyunyiza. Kwa kweli, desturi ya kubadilisha kunyunyiza badala ya ubatizo haikuwahi kusikika hadi mwaka wa A.D. 253 (Thompson na Jackson, 1984, ukurasa 11).
Licha ya ukweli kwamba neno “ubatizo” halihusiani na kunyunyiza, kuna vifungu kadhaa vya Maandiko ambavyo mara nyingi hutumiwa na watetezi wa kunyunyiza ili kuhalalisha msimamo wao.
MAMBO YA WALAWI 14:15-16
Wakati mwingine wale wanaotetea desturi ya kunyunyiza, hudai kwamba njia tatu za kawaida za kisasa za ubatizo (kuzamishwa katika maji, kumimina maji, na kunyunyiza) zote zimeruhusiwa katika Mambo ya Walawi 14:15-16: “Na kuhani atatwaa katika hicho Kikombe cha Mafuta, naye atamimina katika kiganja cha mkono wake wa kushoto. Ndipo kuhani atachovya kidole chake cha kuume katika yale mafuta yaliyo katika kiganja cha mkono wake wa kushoto, naye atanyunyiza baadhi ya yale mafuta kwa kidole chake mbele za Bwana mara saba” (imezistizwa).
Angalia ni kwa namna gani Mambo ya Walawi 14:15-16 ilivyoandikwa kuhusu mchakato wa utakaso wa wenye ukoma baada ya kupona kwao kutokana na ugonjwa wao. Mchakato huu wa utakaso ulikuwa njia ambayo mwenye ukoma aliyepata nafuu ambavyo angeweza kurejea katika jamii ya Kiebrania (Keil na Delitzsch, 1976, 1: 385). Mambo ya Walawi 14:15-16 ni sehemu ya mjadala wa tendo la pili la utakaso wa wenye ukoma. Mchakato huu ni sawa na ule uliotajwa katika Mambo ya Walawi 8:23, wakati ule Musa alipoweka wakfu Aroni na wanawe kuwa makuhani. Mambo ya Walawi 14:15-16 na Mambo ya Walawi 8:23 hayahusiani kabisa na ubatizo wa Agano Jipya (vifungu vyote vinahusu mwongozo wa sheria ya Musa, sio sheria ya Kikristo—tazama Waebrania 7:22-28; Wagalatia 3:21-29), na hivyo haviwezi kutumika kuhalalisha kunyunyiza kama njia inayofaa ya ubatizo.
ISAYA 52:15
Baadhi ya watu wanadai kwamba kwa sababu kifungu hiki kinataja neno “kunyunyiza,” tendo la kunyunyiza lazima liwe mbadala wa kimaandiko kwa ubatizo wa Agano Jipya. Tunapaswa kutathmini uhalali wa madai hayo kwa kuchunguza muktadha wa Isaya 52:15: “Ndivyo atakavyowanyunyizia mataifa mengi; Wafalme watafumba vinywa vyao kwa ajili yake; Kwa maana wataona wasiokuwa wameambiwa, na kuyaelewa wasiyokuwa wamesikia” (imezistizwa). Aya hii imewekewa muktadha katika sehemu ya Maandiko inayojadili dhabihu ya Kristo kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, hivyo ni wazi kwamba Yule Atakayewafanya “mataifa mengi kustaajabu” ni Bwana Mwenyewe.
Neno “kunyunyiza” katika Isaya 52:15 limetafsiriwa kutoka kwenye neno la Kiebrania nazah. Kila mara nazah inapotokea katika Agano la Kale, inatafsiriwa kuwa “kunyunyiza” (katika toleo la King James Versionꟷsoma Kutoka 29:21; Mambo ya Walawi 5:9; Hesabu 8:7), lakini baadhi ya wasomi wanaamini kwamba tafsiri sahihi zaidi ya nazah hapa ni “kustaajabisha” (km., Hailey, 1992, uk. 435; Keil na Delitzsch, 1976, 7: 308). Albert Barnes (1950, 2: 258) alibaini kwamba matumizi ya “kunyunyiza” katika muktadha huu ni ama kielelezo cha kunyunyiza damu katika Agano la Kale (na kiishara kiunganisho kati ya kunyunyiza huko na kumwagika kwa damu ya Kristo msalabani), au kwa kunyunyiza maji ili kuashiria utakaso na usafi (ona Mambo ya Walawi 14:51; Waebrania 9:19). Hata hivyo, kama nazah ingetafsiriwa kwa kumaanisha“kustaajabisha,” msisitizo wa aya hiyo ungebadilika kabisa. Aya hiyo ingetuambia kwamba mateso ya Kristo yangewafanya mataifa “kustaajabisha.” Wengi wanakubali tafsiri hiyo kwa sababu ya kauli katika aya ya 15, “Wafalme watafunga vinywa vyao.” Tafsiri hii inaonesha kwamba wengi wangeweza kushangazwa au hata kunyamaza kimya wakati Neno lilipokuwa mwili, kufa kama dhabihu kwa ajili ya dhambi, na kufufuka kutoka kwa wafu (Hailey, 1992, ukurasa 436; Jackson, 1991, ukurasa 105). Bila kujali ni tafsiri gani ya nazah ni sahihi katika muktadha huu, hakuna kitu kilicho katika Isaya 52:15 kinachohusiana na ubatizo wa Agano Jipya, hivyo hakiwezi kutumika kuhalalisha desturi ya kisasa ya kunyunyiza.
EZEKIELI 36:25
Wale wanaopendekeza kwamba kunyunyiza ni mbadala halali wa ubatizo wakati mwingine wanarejea Ezekieli 36:25 kama “andiko la ushahidi.” “Nami nitanyunyiza maji safi juu yenu, nanyi mtakuwa safi; nitawatakasa na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote” (imeelezwa). Hata hivyo, aya hii haiko katika muktadha unaohusu ubatizo. Utafiti wa Ezekieli 35 unaonesha kwamba, kuhusu lugha “kuosha” ni dhahiri methali. Ingekuwa methali inayofaa kwa Ezekieli kutumika katika kuhusiana na wasikilizaji wake, kwa sababu ya mfumo wa Musa wa utakaso. Vifungu vya Agano la Kale vinavyotumia lugha kama ile inayotumika hapa kuhusu “kuosha” ni vingi. Kwa mfano, Musa aliandika katika Kutoka 30:20: “Watakapoingia hemani mwa kukutania, au watakapoikaribia madhabahu kuhudumu, ili kufukiza sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana, wataosha maji, wasife.” Kutoka 29:4 inasomeka: “Nawe utawaleta Aroni na wanawe kwenye mlango wa hema ya kukutania, nawe utawaosha kwa maji.” Hesabu 19:18 inafafanua: “Na mtu aliye safi atatwaa hisopo, aichovye ndani ya maji, na kuinyunyiza kwenye hema, na vyombo vyote, na watu waliokuwamo, na yule aliyegusa mfupa, aliyeuawa, aliyekufa, au kaburi.” Wazo la kunyunyiza na kuosha limeenea katika vifungu vya Agano la Kale, lakini katika vifungu hivyo (kama vile Ezekieli 36), ubatizo kwa ajili ya wokovu hauzingatiwi. Kinachozungumziwa katika Ezekieli 36 ni, kwa maana halisi, uharibifu wa mmoja wa maadui wa Israeli, taifa la Edomu, na kwa maana ya mfano, uharibifu wa baadaye wa maadui wote wa Bwana (Jackson, 2002a, ukurasa 31).
Angalia Ezekieli 36:24: “Kwa maana nitawachukua kutoka katika mataifa, na kuwakusanya kutoka katika nchi zote, na kuwaleta katika nchi yenu wenyewe.” Kisha, mara moja kufuatia aya inayotaja kunyunyiza maji safi, Mungu alisema: “Nami nitawapa moyo mpya, na kuweka roho mpya ndani yenu; nami nitatoa moyo wa jiwe miilini mwenu, na kuwapa moyo wa nyama” (Ezekieli 36:26). Aya hizi mbili zinawasilisha muktadha wa karibu ambao watu wengi wa kidini wa kisasa wanachukua Ezekieli 36:25 ili kuhalalisha kunyunyiza. Ikiwa tunapaswa kuamini kwamba Ezekieli alikuwa akiandika kuhusu hali halisi ya kunyunyiza maji katika aya hii, basi tungekuwa pia na maana ya kuelewa matumizi ya Ezekieli ya “moyo wa jiwe” katika aya ya 26 kama kuwa halisi. Ubatizo wa Agano Jipya hauzingatiwi katika Ezekieli 36:25. Wayne Jackson alibainisha kwamba wasomi wengi wa kimadhehebu wanaotetea desturi ya kunyunyiza kama aina halisi ya ubatizo hawataji Ezekieli 36:25, kwa sababu mstali huo hausaidii madai yao (2002, ukurasa 31). Mbadala wa kunyunyiza kwa ubatizo wa kweli hauwezi kutetewa, kwa kuzingatia Ezekieli 36:25.
MATENDO 2:41
Wakati mwingine, wale wanaokubali kunyunyiza wanarejelea Matendo 2 wakijaribu kuhalalisha msimamo wao. Baadhi yao wanasema kwamba mitume kumi na wawili wasingeweza kuzamisha watu wapatao 3,000 kwa siku moja (Matendo 2:41 yanarekodi kwamba “takriban roho elfu tatu” walibatizwa siku ya Pentekoste), hivyo mitume walilazimika kunyunyiza maji juu ya wale 3,000. Hata hivyo, kama kila ubatizo ungetumia takriban dakika moja, mitume wangeweza kumaliza kazi hiyo kwa zaidi ya saa nne tu (Jackson, 2002, ukurasa 32). Pia, hakuna kifungu chochote katika Agano Jipya kinachodai kwamba mitume walilazimika kufanya ubatizo wote wenyewe.
Wengine wanadai kuwa hakukuwa na maji ya kutosha Yerusalemu kuweza kuhudumia kwa kuzamishwa mwili wote. Hata hivyo, kulikuwa na mabwawa mengi huko Yerusalemu, mengine yakiwa makubwa. Bwawa la Bikira lilikuwa na ukubwa wa miguu 132 za mraba na urefu wa futi tatu. Bwawa la Siloamu lilikuwa na ukubwa wa futi 800 za mraba, na lilikuwa na kina cha zaidi ya futi tatu. Gihoni ya Chini ilikuwa na zaidi ya eka tatu, na ingeweza kuwa na kina cha futi ishirini za maji; zaidi ya hayo, kulikuwa na mabwawa mengine (McGarvey, 1881,ukurasa 201). Bila shaka, siku ya Pentekoste, waumini walizamishwa.
1 WAKORINTHO 10:2
Wale wanaounga mkono mbadala wa kunyunyiza kwa ubatizo wakati mwingine wanarejelea 1 Wakorintho 10:2 kwa kuhalalisha msimamo wao. Kifungu hicho kinaeleza kwamba “wote walibatizwa na Musa katika wingu na katika bahari”—rejeo la moja kwa moja Kutoka 14:22. Ubatizo wa Musa ni tofauti kabisa na ubatizo wa Kristo, lakini baadhi ya wale wanaotetea kunyunyiza wanadai kwamba, kwa kuwa Paulo alinena kuhusu kuvuka Bahari Nyekundu “ubatizo,”. Ni lazima Waisraeli walinyunyiziwa walipoivuka Bahari Nyekundu. [Israel hakika hawakuzamishwa ndani ya maji—watu walitembea kwenye nchi kavu (Waebrania 11:29).] Paulo alimaanisha nini aliposema kwamba baba zetu “walibatizwa kuwa Musa”?
Maana ya ubatizo katika 1 Wakorintho 10:2 ni halisi na wa mfano. Waisraeli walibatizwa—kwa maana ya kwamba walizungukwa na maji, ingawa maji hayakuwagusa. Haya ni matumizi halali ya neno “ubatizo.” Kwa mfano, wakati mwili uponazikwa kwenye kaburi, mwili “unazamishwa” ardhini (umefunikwa na uchafu), ingawa jeneza linauzuia uchafu kugusa mwili. Kwa maana hiyo, watoto wa Israeli walizamishwa katika Bahari Nyekundu. Pia Paulo aliandika kuhusu ubatizo kwa maana ya kifigurishi: watoto wa Israeli walibatizwa na Musa kwa maana kwamba walijitolea kwa uongozi wake na, kupitia yeye, uongozi wa Mungu. G.G. Findlay alieleza:
Wingu, likiwapa kivuli na kuwaongoza Waisraeli kutoka juu, na ‘bahari’ ikiwafungulia njia kupitia katikati na kuzamisha maadui zao nyuma yao,hayo yote ilikuwa ishara za utukufu kwa ‘baba zetu’ za wokovu wa Mungu; kwa pamoja yalifanyika ili kuoshwa kwa kuzaliwa upya (Tito 3:5),hii ikianzisha maisha ya agano la taifa; walipokanyaga njia ya miujiza kati ya maji ya juu na ya chini, Israeli ilizaliwa katika hali yake ya Kimungu. Hivyo ‘wote walipokea ubatizo wao kwa Musa, wakiingia kupitia yeye katika ushirika ulioeleweka na Mungu; hata hivyo Wakorintho katika matumizi ya kipengele hicho cha kiishara walikuwa wamebatizwa kwa Kristo (Warumi 6:3, Wagalatia 3:27; ukurasa 857).
Ubatizo katika Kristo haujaagizwa katika kitabu cha Kutoka 14:22, ingawa mfano wa kuvuka Bahari ya Shamu unatoa kiashiria cha ubatizo katika Kristo kwa njia ya mfano, kama vile safina ya Nuhu (1 Petro 3:20-21; tazama Lenski, 1937, ukurasa 391). Hata hivyo, katika kitabu cha Kutoka 14, watoto wa Israeli walivuka Bahari Nyekundu ili kuokoa maisha yao ya kimwili, sio kuokoa roho zao za milele, na “ubatizo” wa katika kitabu cha Kutoka 14 ulianzishwa na Musa, maelfu ya miaka kabla ya ubatizo wa Kristo kuanza kutumika. Hakuna utambulisho wa “njia” sahihi ya ubatizo katika 1 Wakorintho 10:2 au Kutoka 14:22, hivyo mbadala wa kunyunyiza kwa ubatizo hauwezi kutetewa kwa kuzingatia vifungu vyote viwili.
WAEBRANIA 10:22
Aya hii mara nyingi inatajwa kama uthibitisho kwamba watu wanapaswa kunyunyiziwa ili kuokolewa, lakini uchunguzi mfupi wa maandiko unaonesha maana nyingine. Waebrania 10:22 inasema: “Na tumkaribie Mungu kwa moyo wa kweli, katika utimilifu wa imani,ili hali mioyo yetu ikiwa imenyunyiziwa safi kutoka kwenye dhamiri mbaya na miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi” (imeelezwa). Aya hii inaonekana kuchota maana yake ya kiroho kutoka katika agano la zamani la Mungu na Israeli. Katika kipindi hicho cha sheria ya Musa, makuhani wakuu walipaswa kujiosha wenyewe kabla ya kuingia Mahali Patakatifu Zaidi (angalia Mambo ya Walawi 16:3-4). Angalia Waebrania 10:19-21: “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kuingia Patakatifu pa damu ya Yesu, kwa njia mpya na iliyo hai aliyoifungua kwa ajili yetu, kupitia pazia, yaani, mwili wake, na kuwa na Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu….” Aya hizi, na aya ya 22, zote zinahusiana na jinsi gani watu wanavyokaribia kwa Mungu, na ujumbe katika aya ya 22 uko wazi: mioyo yetu lazima iwe ya kweli. Kinachowezekana kufanya mioyo yetu iwe ya kweli ni “kunyunyiza” kwa mioyo yetu. Ikiwa mioyo ya Wakristo inanyunyiziwa, “dhamiri mbaya” inaondolewa na haibebi tena hatia ya dhambi. Dhamiri mbaya ni ile isiyokataa mabaya (1 Timotheo 4:2). Robert Milligan alielezea hivi:
Kila tendo tunalofanya kinyume na mapenzi ya Mungu tunayoyajua lina najisi dhamiri yetu na pia ufahamu wetu; tunayo dhamiri mbaya na ufahamu mbaya. Na hii, ilimradi inabaki, lazima itavuruga muungano, ushirika, na ushirikiano wetu na Mungu. Mtoto anayeteseka na dhamiri mbaya kwa sababu ya kuvunja mapenzi ya baba yake anayoyajua hawezi, maadamu hisia hiyo inabaki, kumkaribia kwa ujasiri kamili. Lakini anapotubu ubaya huo, kukiri kosa, na kujua kwamba kosa limeondolewa, basi ni mabadiliko gani yanakuja juu yake (1950, ukurasa 281).
Mwandishi wa Kiebrania alifanya rejeo kwenye ubatizo, lakini angalia jinsi alivyoifanya. Aya ya 22 inasema mioyo yetu imenyunyiziwa kutoka kwenye dhamiri mbaya, lakini miili yetu imeoshwa kwa maji safi. Kunyunyiza kwa hakika kunazingatiwa katika Waebrania 10:22, lakini msomaji lazima awe makini kuona ni nini hasa kinachonyunyiziwa. Katika kifungu hiki, mwandishi wa Waebrania anaonesha haja ya kunyunyiziwa mioyo yetu, hivyo ni wazi maana si halisi, bali lazima ieleweke kuwa ya mfano au ya tamathali. Sehemu pekee ya aya inayoweza kuelezea maji halisi ni ile sehemu inayotaja “kuoshwa.” Kuoshwa huku ni nini? Ni ile “kuoshwa kwa kuzaliwa upya”tendo linalotajwa katika Tito 3:5—ubatizo (Milligan, 1950,ukurasa 282). Hata hivyo, sehemu ya aya inayofafanua kunyunyiza, haihusiani na sehemu ya aya inayofafanua ubatizo. Mioyo ya Wakristo inanyunyiziwa kwa ishara na damu ya Kristo, lakini miili yao inaoshwa (inazikwa ndani ya maji kwa msamaha wa dhambi zao; angalia Matendo 22:16; Marko 16:16). Mazoezi ya kisasa ya kunyunyiza kwa ubatizo hayajaidhinishwa na Waebrania 10:22.
UBATIZO WA KWELI
Ikiwa “mistari ya uthibitisho” ya kunyunyiza kama mbadala wa ubatizo haithibitishi kwamba kunyunyiza ni aina ya ubatizo, basi ni nini aina halisi ya kibiblia ya ubatizo? Ubatizo ambao Yesu aliidhinisha na kuamuru ni ule unaooneshwa wazi na neno la Kiyunani baptizo: kuzamishwa. Kitabu cha Matendo kimejaa hadithi za ubatizo, na katika kila mfano, muhitaji wa ubatizo alizamishwa. Katika kila mfano, kuzamishwa huko kulitosha (tazama Matendo 10:48; Matendo 16:31-33; Matendo 22:16).
MAREJELEO
Arndt, William, F.W. Gingrich, and Frederick W. Danker (1979), A Greek-English Lexicon of the New Testament and Other Early Christian Literature (Chicago, IL: University of Chicago Press), second edition revised.
Barnes, Albert (1950), Notes on the Old Testament: Isaiah (Grand Rapids, MI: Baker).
Findlay, G.G. (no date), The Expositor’s Greek Testament, ed. W. Robertson Nicoll (Grand Rapids, MI: Eerdmans).
Hailey, Homer (1992), A Commentary on Isaiah (Louisville, KY: Religious Supply).
Jackson, Wayne (1991), Isaiah: God’s Prophet of Doom and Deliverance (Abilene, TX: Quality).
Jackson, Wayne (2002a), “Did The Prophet Ezekiel Preview ‘Sprinkling’ As A Form of New Testament ‘Baptism’?,” Christian Courier, 38:31, January.
Jackson, Wayne (2002b), “Notes from the Margin of My Bible,” Christian Courier, 38:31, January.
Keil, C.F. and F. Delitzsch (1976a reprint), Commentary on the Old Testament (Grand Rapids, MI: Eerdmans).
Lenski, Robert C.H. (1937), The Interpretation of I and II Corinthians (Minneapolis, MN: Augsburg).
Martin, Luther W. (1991) “Translating Baptizo,” Firm Foundation, 106:208-210, July.
McGarvey, J.W. (1881), Lands of the Bible (Philadelphia, PA: Lippincott).
Milligan, Robert (1950), The New Testament Commentary: Epistle to the Hebrews (Nashville, TN: Gospel Advocate).
Thayer, J.H. (1958 reprint), A Greek-English Lexicon of the New Testament (Edinburgh: T. & T. Clark).
Thompson, Bert and Wayne Jackson (1984), “That ‘Loaded’ Questionnaire,” [On-line], URL: https://www.apologeticspress.org/articles/1181.
UZALISHAJI & MASHARTI: Tunayo furaha kutoa ruhusa ya makala hii kuzalishwa kwa sehemu au kwa ukamilifu, ili mradi masharti yetu yazingatiwe.
Masharti ya Uzalishaji→
REPRODUCTION & DISCLAIMERS: We are happy to grant permission for this article to be reproduced in part or in its entirety, as long as our stipulations are observed.